Kiongozi Mbio za Mwenge awafagilia RUWASA Mtwara

MTWARA; KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2024, Godfrey Mnzava ameelezwa kufurahishwa na namna ambavyo Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya Mtwara wanavyotekeleza miradi ya maji kwa kufuata taratibu zinazotakiwa.

Akizungumza mara baada ya Mwenge wa Uhuru kukagua mradi wenye thamani ya Sh milioni 600 unaojengwa Kijiji cha Makome, Kata ya Mbawala, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara, Mnzava amesema hatua hizo zimesaidia kuhakikisha ufanisi kwenye utekelezaji wa mradi.

“RUWASA Wilaya ya Mtwara wamefuata taratibu sheria ipasavyo kwenye matumizi ya fedha na hata upatikanaji wa mzabuni, jambo ambalo limeonesha ufanisi mkubwa kwenye utekelezaji wa mradi,” amesema.

“Tunapofika katika eneo ambalo mmemtendea haki Mheshimiwa Rais maneno yanakuwa sio mengi, hapa tumeridhika na Mwenge wa Uhuru tutaweka jiwe la Msingi kama ishara ya kwamba tumeridhika,” amesema.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo ameeleza kufurahishwa na hatua ya wakala huo kutoa huduma ya maji kwa wananchi huku ujenzi wa mradi ukiwa unaendelea.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mtwara, Hamisi Masindike amesema mradi huu umezingatia sera ya Maji ya kumtua mama ndoo kichwani na kuzingatia umbali usiozidi mita 400 kutoka kituo moja hadi kingine cha kuchota maji.

Mradi umelenga kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi kutoka asilimia 67.2 mpaka kufikia asilimia 68.2 2024 kwa Wilaya ya Mtwara.

 

Habari Zifananazo

Back to top button