Prof Mkumbo: Rais anaenda nje kutafuta fursa, sio misaada

DODOMA: Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kufanya ziara za nje kwa lengo la kutafuta fursa za biashara na uwekezaji badala ya misaada, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 bungeni.
“Mheshimiwa Rais anaenda nje kutafuta fursa za biashara na uwekezaji, na sio kutafuta misaada,” alisema Profesa Mkumbo, akieleza mkakati wa Serikali wa kujenga uchumi unaochochewa na uwekezaji, biashara na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.
Kauli hiyo imekuja wakati Serikali ikiweka uwekezaji na biashara miongoni mwa sekta muhimu zitakazoongoza mageuzi ya uchumi katika mwaka wa fedha 2026/27.
Kwa mujibu wa mpango huo, Serikali inalenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kugharamia na kutekeleza miradi ya maendeleo, huku ikiendelea kutafuta washirika wa biashara na uwekezaji kutoka masoko mbalimbali duniani.
Profesa Mkumbo ameliambia bunge kuwa mkakati huo unalenga kuvutia mitaji, teknolojia na utaalamu utakaosaidia kuongeza uzalishaji, kuimarisha ushindani wa uchumi na kufungua fursa zaidi za ajira kwa Watanzania.
Hatua hiyo inaonyesha mabadiliko ya msisitizo wa Serikali kutoka utegemezi wa misaada kuelekea uchumi unaojengwa kupitia uwekezaji, biashara na uzalishaji wa ndani.



