Changamoto ya maji safi kumalizika Mbogwe

WAKALA wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Mbogwe ipo mbioni kukamilisha mradi wa maji Ushirika- Mlale ili kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi kwa wananchi wapatao 21,009.

Wanufaika wa mradi ni wakazi wa vijiji vya Ikobe, Isebya, Ushirika, Mlale, Kadoke na Ushetu na chanzo chake ni visima virefu vyenye wastani wa mita 84 na uwezo wa kutoa lita 20,300 kwa saa kupitia nishati ya umeme.

Mradi huu ulianza kutekelezwa Aprili, 2024 na unatarajia kukamilika Aprili, 2025 chini ya mkandarasi OTONDE CONSTRUCTION & GENERAL SUPPLIES LIMITED wa jijini Mwanza kwa gharama ya Sh bilioni 2.

Meneja wa Ruwasa wilayani Mbogwe, Mhandisi Rodrick Mbepera ameeleza hayo katika taarifa yake kwa viongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2024 na tayari mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni 1.3.

SOMA: Upatikanaji maji safi vijijini wafikia asilimia 79

Amesema katika bajeti ya mwaka 2023/24 Ruwasa imetekeleza ujenzi wa miundombinu ya maji kwa kujenga mtandao wa bomba wenye urefu wa Km 30.57 kati ya Km 50.059 pamoja na ujenzi wa matenki matatu.

Mhandisi Mbepera amesema tenki la kwanza lina uwezo wa ujazo wa maji wa lita 150,000, tenki la pili lina ujazo wa lita 75,000 huku tenki la tatu lina ujazo wa lita 50,000.

“Wananchi wa Ikobe, Isebya, Ushirika, Mlale, Kadoke na Ushetu wamehamasika na ujenzi wa mradi huu wa maji na wameweza kutoa maeneo yao yenye thamani ya shilingi milioni 24 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji,”.

“Kabla ya mradi huu wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanatumia maji ya visima vifupi ambayo kimsingi siyo salama,” amesema Mhandisi Mbepera.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Geita, Rose Busiga ameishukuru serikali kwa mradi huo kwani utaongeza uhakika wa huduma ya maji safi na salama na kuwezesha wananchi kuendelea kuwa na imani na serikali yao.

SOMA: Aweso aonya mfumo wa GePG huduma za maji

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2024, Godfrey Mzava amesema lengo la serikali ni kuona wananchi wanapata huduma ya maji safi kwa wakati hivo ni lazima miradi yote ikamilishwe kwa usanifu kama ilivyopangwa.

Habari Zifananazo

Back to top button