Dk Samia kuongoza kikao afya ya mama, mtoto

DAR ES SALAAM: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kinara wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajia kuwaongoza viongozi wakuu wa nchi za Afrika na wadau wa maendeleo katika kujadili na kuhamasisha uwekezaji katika afya ya uzazi, mama, mtoto mchanga na mtoto barani Afrika.
–
Kikao hicho cha ngazi ya juu kinatarajiwa kufanyika Septemba 23, 2026, jijini New York, Marekani, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA-81).
–
Rais Samia atakuwa mwenyeji wa kikao hicho katika nafasi yake ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto.
–
Miongoni mwa matokeo yanayotarajiwa ni kupitishwa kwa tamko rasmi la kuharakisha hatua za kukomesha vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama, mtoto mchanga na mtoto, pamoja na kutangazwa kwa ahadi za uwekezaji kutoka kwa nchi na washirika wa maendeleo.
–
Uongozi wa Tanzania katika ajenda ya afya ya uzazi, mama na mtoto umejengwa kupitia utashi wa kisiasa, uwajibikaji na hatua zinazolenga kuboresha huduma za afya kwa wanawake na watoto.
–
Hatua hiyo inaendeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha masuala ya afya ya uzazi, mama na mtoto yanaendelea kupewa kipaumbele, huku Tanzania ikiwa sehemu ya juhudi za Bara la Afrika katika kuharakisha upatikanaji wa huduma bora na salama kwa wanawake na watoto ifikapo mwaka 2030.



