Kamati kuchunguza mkataba jezi Taifa Stars

DAR ES SALAAM: Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, anakusudia kuunda kamati ya kuchunguza mkataba wa mzabuni wa jezi za timu za taifa ili kubaini manufaa ya mkataba huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Zaituni Mkwama, Kamati hiyo itachunguza mkataba huo pamoja na fursa ya mauzo ya jezi za timu za taifa zinazoweza kuchangia katika uendeshaji wa timu hizo.

Mkwama amesema Waziri Makonda hatambui matangazo ya jezi mpya za timu za taifa kutokana na mchakato wa kuzibadilisha kutohusisha wizara, licha ya maelekezo aliyoyatoa Februari 2026.
Amesema katika maelekezo hayo, Waziri Makonda alielekeza kuboreshwa kwa jezi za timu za taifa ili ziakisi manufaa mapana kwa nchi, ikizingatiwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi katika maandalizi ya timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.



