Kigogo FOA Motors mbaroni akidaiwa kutapeli Sh Mil 150

Kigogo FOA Motors mbaroni akidaiwa kutapeli Sh Mil 150

JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa, linamshikilia Michael Mbata (34), mfanyabiashara mkazi wa Dar es Salaam kwa tuhuma ya kujipatia Sh Milioni 150 kwa njia ya udanganyifu.

Akizungumza na wanahabari leo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, alisema mtuhumiwa huyo alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Abdallah Huwel na Isaya Edward, wote wakazi wa Iringa.

Wakati Huwel alitapeliwa Sh Milioni 100 kwa ahadi ya kuagiziwa gari aina ya Howo, Bukumbi alisema Edward naye alitapeliwa Sh Milioni 50 kwa ahadi ya kununuliwa aina hiyo hiyo ya gari.

Advertisement

“Mtuhumiwa huyo aliwatapeli watu hao kwa ahadi ya kuwaagizia magari hayo kutoka Japan na Uingereza kupitia kampuni yake ya FOA Motors iliyopo Dar es Salaam,” alisema.

Baada ya kupatiwa fedha hizo Kamanda Bukumbi, alisema mtuhumiwa huyo amekuwa akipoteza mawasiliano na watu hao kabla ya Agosti 20, mwaka huu kukamatwa akiwa katika eneo la Chanika jijini Dar es Salaam na kuletwa Iringa waliko walalamikaji hao.

“Baada ya kukamatwa na kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake alikutwa na magari mawili ambayo ni Nissan Dualis namba T 104 DZL lenye thamani ya Sh Milioni 24 na Subaru impreza namba T 328 DZR lenye thamani ya Sh Milioni 18,” alisema.

Alisema jeshi lake limekamilisha upelelezi na wakati wowote kuanzia sasa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.

Kamanda Bukumbi alitoa tahadhari kwa umma wa Watanzania, kuwa makini na mkurugenzi huyo wa kampuni hiyo ya FOA Motors Ltd,  ili kujiepusha kuingia kwenye mtego wa kutapeliwa.