‘LadyMaa’ afunguka viongozi, watu maarufu kutumia biadhaa za ndani

DAR ES SALAAM: VIONGOZI, watu maarufu na wanamitindo nchini wametakiwa kuwapa kipaumbele wafanyabiashara wazawa kwa kutumia bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa ndani ya nchi, hatua itakayosaidia kukuza uchumi pamoja na kulinda ushindani wa haki sokoni.

Wito huo umetolewa na mfanyabiashara wa bidhaa za urembo kwa wanawake, Mariam Bakari Salum maarufu ‘LadyMaa’, ambaye amesema matumizi ya bidhaa za ndani yana mchango mkubwa katika kuongeza ajira kwa vijana na wanawake wanaojihusisha na shughuli mbalimbali za urembo.

Amesema sekta ya urembo imekuwa ikikua kwa kasi nchini Tanzania, hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa jamii kuamini na kuunga mkono biashara za wazawa badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje ya nchi pekee.

“Tunapowaunga mkono wafanyabiashara wa ndani tunasaidia fedha kubaki kwenye mzunguko wa uchumi wetu, lakini pia tunafungua nafasi za ajira kwa wasusi, wauzaji na wasambazaji wa bidhaa mbalimbali za urembo,” amesema LadyMaa.

LadyMaa ambaye duka lake lipo Sinza Kijiweni, Dar es Salaam, amesema biashara yake imejikita katika kuuza mawigi ya kisasa, nywele za natural hair, hair products mbalimbali pamoja na vifaa vya accessories za nywele kwa wanawake wa rika tofauti.

Ameeleza kuwa bidhaa hizo zinasaidia wanawake kuboresha mwonekano wao, kuongeza kujiamini pamoja na kupata huduma bora zinazokwenda sambamba na mahitaji ya sasa ya ulimwengu wa urembo.

Mbali na hilo, amesema mafanikio ya biashara yoyote hutegemea zaidi ubora wa bidhaa pamoja na namna mfanyabiashara anavyojenga uaminifu kwa wateja wake.

Amesema kwa muda mrefu amekuwa akihakikisha anatoa huduma bora na bidhaa zenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya wateja wa aina tofauti, jambo lililomsaidia kujenga jina kwenye biashara hiyo.

Akizungumzia uzoefu wake wa kuwahudumia wabunge na viongozi mbalimbali, LadyMaa amesema watu hao hutumia muda mwingi kwenye mikutano, vyombo vya habari na mbele ya kamera, hivyo huhitaji mwonekano wenye kuvutia muda wote.

“Kazi zao zinawafanya wawe mbele ya watu kila mara, hivyo wanahitaji kuonekana nadhifu na tofauti. Hilo pia linawafanya kuamini zaidi huduma zetu za ndani,” amesema.

Aidha, amesema watu maarufu wanapochagua kutumia bidhaa za wazawa huongeza thamani ya biashara hizo kwa kuwa jamii nyingi huamini vitu vinavyotumiwa na viongozi, wasanii au watu wenye ushawishi mkubwa.

Kwa mujibu wa LadyMaa, hali hiyo imekuwa msaada mkubwa katika kuitangaza biashara yake kwani baadhi ya wateja wamekuwa wakifika dukani kwake baada ya kuona huduma zake zikitumiwa na watu maarufu.

Amesema changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara wengi wa ndani ni ushindani kutoka kwa bidhaa za nje pamoja na baadhi ya wananchi kuamini zaidi bidhaa zinazoagizwa kutoka mataifa mengine.

Kutokana na hali hiyo, amewashauri wafanyabiashara wazawa kuhakikisha wanazingatia ubora, huduma nzuri kwa wateja na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuweza kuhimili ushindani wa soko la sasa.

Mbali na biashara, LadyMaa amesema ana ndoto ya kuwainua wanawake na vijana zaidi kupitia mafunzo ya urembo na biashara ili waweze kujitegemea kiuchumi.

“Biashara inaweza kubadilisha maisha ya mtu kama ataamua kuwa mvumilivu, mwaminifu na mwenye kujituma. Vijana wengi wanapaswa kutumia fursa zilizopo kwenye sekta ya urembo,” amesema.

LadyMaa ni miongoni mwa wafanyabiashara wanawake waliofanikiwa kujijengea jina katika biashara ya urembo nchini Tanzania, huku akiendelea kutoa huduma zake za mawigi, natural hair, hair products na accessories za nywele katika eneo la Sinza Kijiweni, Dar es Salaam.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button