Mama lishe Kurasini wapatiwa elimu nishati safi

DAR ES SALAAM: MAMA na Baba lishe wa eneo la Kurasini lililopo Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam wamepatiwa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia mkaa mbadala, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati salama.
Katika elimu hiyo, washiriki wameelekezwa namna ya kutumia mkaa mbadala ambao unauwezo wa kudumu kwa saa sita ukiwa kwenye matumizi ya upishi wa vyakula mbalimbali, pamoja na majiko ya umeme yenye uwezo wa kutumia umeme mdogo, na uwezo wa kupika vyakula mbalimbali.
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umetoa elimu hiyo kwa kushirikiana na Ecopower ambapo mama na baba lishe wamehimizwa kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia kutokana na umuhimu wake katika kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Uendeshaji PBPA, Bruno Tarimo, amesema wameamua kuwafikia mamalishe kwa kuwa kundi hilo linahudumia idadi kubwa ya watu wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya Kurasini na Kigamboni.
Amesema wafanyakazi wengi huondoka majumbani asubuhi na kurejea usiku, hivyo hutegemea chakula kinachopatikana katika maeneo ya mamalishe, jambo linalofanya kundi hilo kuwa muhimu katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Kwa kuwafikia mamalishe, tunawafikia watu wengi zaidi. Wateja wao wanapoona chakula kimepikwa kwa kutumia nishati safi, wanaweza pia kupata elimu na kwenda kuwafikishia ndugu, jamaa na marafiki,” amesema Tarimo.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, hivyo kila mdau anapaswa kushiriki katika kufanikisha azma hiyo.
Tarimo amesema katika zoezi hilo mamalishe wamepewa elimu kuhusu matumizi ya majiko mbalimbali mbadala, ikiwemo majiko ya umeme na majiko banifu yanayopunguza matumizi ya nishati na uzalishaji wa moshi.
Amesema matumizi ya kuni na mkaa yanaweza kuwa na madhara kwa afya ya watumiaji pamoja na mazingira, hivyo matumizi ya nishati safi yatasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na madhara ya kiafya.
“Tunapunguza madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya nishati chafu, lakini pia tunasaidia kupunguza gharama ambazo Serikali hutumia katika matibabu ya magonjwa yanayohusiana na uchafuzi wa hewa,” amesema.
Aidha, Tarimo amewashukuru wadau walioshiriki katika zoezi hilo, akiwemo Kikundi cha Jitihada pamoja na uongozi wa Mamalishe Tanzania, kwa kushirikiana katika kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Pia wamegawa wamegawa tani .1.75 za mkaa mbadala kwa amama na baba lishe 70 wa kikundi cha Jitihada.
Aidha, Rais wa Mama Lishe Tanzania, Latifa Habibu Masasi, amesema upatikanaji wa gesi, majiko ya umeme, majiko banifu na mkaa mbadala umewapa mama lishe fursa ya kuchagua teknolojia inayokidhi mahitaji na uwezo wao wa kiuchumi.
Amesema matumizi ya nishati safi ni muhimu katika kuboresha shughuli za biashara ya chakula, kwa kuwa teknolojia hizo zinawawezesha mama lishe kupika kwa haraka, kwa wakati na katika mazingira salama zaidi.
“Nishati safi ni muhimu sana. Teknolojia hizi zinaongeza thamani katika mnyororo wa biashara ya chakula kwa sababu zinawawezesha mama lishe kupika kwa haraka, kwa wakati na katika mazingira salama zaidi,” amesema Masasi.
Amesema mafunzo hayo yanaashiria kuanza kwa kampeni ya PBPA kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia miongoni mwa mama na baba lishe nchini.

Kwa mujibu wa Masasi, kampeni hiyo inatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine yenye mama na baba lishe wanaotoa huduma za chakula kwa wadau wa PBPA, kwa lengo la kuongeza uelewa na matumizi ya nishati safi ya kupikia.



