Marekebisho ya sheria yawapa tabasamu wafugaji

DODOMA; Serikali imewasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283, ili kuweka masharti kuhusu uhifadhi, usimamizi, ulinzi na matumizi endelevu ya wanyamapori.
Sheria hiyo ni miongoni mwa sheria saba zilizopo kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 wa Mwaka 2026 uliowasilishwa leo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari.
Kwa mujibu wa Johari , marekebisho ya sheria hiyo yana vifungu vinavyopendekezwa kuiondoa mifugo miongoni mwa vitu vinavyoweza kutaifishwa baada ya mtu kutiwa hatiani kwa kutenda kosa chini ya sheria.
“Sheria hii ilitungwa mwaka 2009 kwa lengo la kuweka masharti kuhusu uhifadhi, usimamizi, ulinzi na matumizi endelevu ya wanyamapori na bidhaa za wanyamapori.
“Tangu kutungwa kwake, sheria hii imerekebishwa mara kadhaa kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa masharti mbalimbali ya sheria.
“Vifungu vya 111 na 116 vinapendekezwa kurekebishwa kwa kuiondoa mifugo miongoni mwa vitu ambavyo vinaweza kutaifishwa baada ya mtu kutiwa hatiani kwa kutenda kosa chini ya sheria.
“Lengo la marekebisho yanayopendekezwa ni kuweka uwiano kati ya kosa na adhabu inayotolewa ili kuimarisha misingi ya haki,” amesema Johari.
Muswada huo unapendekeza marekebisho katika Sheria Kuu Saba, ambazo ni Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Sura ya 116, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287; Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288.
–
Nyingine ni Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa, Sura ya 61, Sheria ya Mamlaka ya Nchi Katika Umiliki wa Mali na Rasilimali Asilia, Sura ya 449; Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini, Sura ya 138; na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283. Bunge limepitisha muswada huo.




Thanks to my father who told me regarding this weblog, this blog is actually amazing.