Mkasiwa: Wanawake wanaweza kuongoza

WAKATI wengi wakiamini nafasi ya utemi ni ya wanaume pekee, Mkoa wa Tabora unaendelea kuhifadhi historia ya kipekee kupitia Mtemi wa Kike wa Watambikolo wa Manyema, Mkasiwa, anayefahamika kwa jina la kuzaliwa Zuhura Musa Osanto.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Dailynews Digital mjini Tabora, Mkasiwa amesema hakuchaguliwa na wananchi kuwa mtemi, bali alirithi nafasi hiyo kupitia ukoo wa kifalme wa mababu zake kwa kufuata taratibu za mila na desturi.

Amesema baada ya kufariki kwa viongozi wa jadi wa ukoo wao, wazee wa mila walifanya tambiko na kubaini kuwa uongozi huo ulipaswa kuendelea kupitia mrithi halali wa familia hiyo. “Utemi si nafasi ya kugombea wala kujitangaza. Ni urithi unaotokana na ukoo unaotambulika kwa mujibu wa mila na desturi,” amesema.

Akizungumzia alama za uongozi wake, Mkasiwa amesema mavazi, vilungu na mapambo anayovaa ni ishara ya mamlaka na utambulisho wa mtemi huku baadhi ya mapambo hayo yakitokana na viumbe wa Bahari ya Hindi na kurithishwa kwa vizazi. Amesisitiza kuwa uwezo wa kuongoza haupaswi kupimwa kwa jinsia, akieleza kuwa wanawake wanaweza kuongoza kwa hekima na busara kama wanaume.

Kwa mujibu wake, historia ya Tabora imewahi kushuhudia watawala wanawake walioongoza kwa mafanikio, akiwemo Mtemi Minza na Ngole Mbilingi. Ameeleza kuwa salamu ya “Iminza” inayotumika katika baadhi ya maeneo ya Tabora iliasisiwa kama ishara ya heshima kwa Mtemi Minza.

Mkasiwa ametoa wito wa kuhifadhi mila na desturi zenye manufaa kwa jamii, huku akipinga zile zinazochochea ndoa za utotoni, kuwanyima watoto wa kike elimu na kukwamisha maendeleo ya wanawake. Aidha, amesema taasisi ya utemi inaendelea kuwa na nafasi muhimu katika kuhifadhi historia, maadili na utamaduni pamoja na kusaidia utatuzi wa migogoro ya kifamilia na kijamii.

Uwepo wa Mtemi wa Kike Mkasiwa unaendelea kuwa alama ya historia ya kipekee ya Mkoa wa Tabora ukionesha kuwa uongozi wa jadi unaweza kuendelezwa na wanawake kwa kuzingatia mila, desturi na urithi wa mababu. SOMA: Mtemi wa Wagogo atamba kuita, kusimamisha mvua

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button