Mtemi wa Wagogo atamba kuita, kusimamisha mvua

MTEMI Yassin Biringi wa Dodoma Makulu ambaye alikabidhiwa kiti hicho hivi karibuni, amesema miongoni mwa vitu alivyoachiwa ni mawe ya tambiko yanayotumika kuita mvua pale zinapochelewa na kwamba ana uwezo pia wa kusimamisha mvua.

Biringi ambaye ni Mtemi wa kabila la Wagogo alisema hayo wakati wa mahojiano na HabariLEO.

“Nina uwezo wa kusimamisha mvua na hili huwa nalifanya nikiwa na mavazi maalumu na kuna maneno huwa natamka,” alisema.

Alisema kuwa jamii ya sasa ni ngumu sana kuamini mila na tamaduni za asili lakini akasema hayo yapo.

Alisema amechaguliwa kuwa Mtemi ili kumrithi baba yake, Ali Biringi ambaye sasa ni mgonjwa.

“Mzee ana watoto 57 kwa wake wanane ambapo mimi ni mtoto wa 27, sasa nina miaka 32,” alisema.

Kati ya watoto 57, watoto wa kike ni 32 na wa kiume ni 32, wajukuu 127, vitukuu 98 na virembwe 57.

“Mtoto wake wa mwisho ana miaka minane kwa sababu ya ugonjwa ndio maana hana tena watoto wengine wadogo,” alisema.

“Zamani Chifu yeyote ni lazima aoe wanawake wengi kwa sababu shughuli za uchifu ni nyingi na hupokea wageni wengi, lazima kuwe na watu wa kumsaidia kumudu majukumu mengine kama ya kilimo na ufugaji,” alisema.

Alisema mtemi anapatikana kwenye familia, haangaliwi mtoto mkubwa au mdogo lakini lazima achaguliwe.

“Kuna wazee wa mila, mizimu yenyewe ikuchague ukikubali mzee mwenyewe ndio anaelekezwa na mizimu, akilala anaoteshwa mtu atakayekalia kiti chake ni huyu, baadaye wanakuja kukusimika. Licha ya kuchaguliwa lazima pia uwe na hekima na busara na moyo wa utu ndipo utapewa kiti,” alisema.

Alisema Mtemi anatakiwa kupenda watu wake kwani bila hivyo ataangamiza watu kwa vile roho za chuki, ubinafsi hazitakiwi.

“Unapopewa utemi ujue una mitihani sana na yote unatakiwa uishinde ili uipoze nchi ikae vizuri. Ni mitihani kwa sababu unaongoza watu na makundi mbalimbali ya watu na siku zote sio wote unaowaongoza wanakupenda. Wengine wanakupinga,” alisema.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button