Ujenzi maadili mema ni msingi wa uongozi bora ngazi zote

TAIFA letu Tanzania limezaliwa takribani miaka 61 iliyopita. Kwa hiyo wote wenye umri wa kuzaliwa chini ya hapo hakika ni watoto wa Tanzania.

Mimi hushangaa sana ninapowasikia hao watoto wa Tanzania wanaposema, na aghalabu kwa jazba, kwamba ‘wanaitamani au wanaililia nchi yao Tanganyika’… nchi ambayo ilidumu kama taifa kwa takribani miaka mitatu tu.

Nina kumbukumbu ya Baba wa Taifa akizungumza na tukiwa tunamsikiliza akisema: “Mambo ya maana ya msingi tuliyowarithisha mnayaacha. Mambo ya ovyo mnayakumbatia… Mtu mwenye akili akikushauri jambo la kipumbavu ukalikubali, anakudharau”.

Nionavyo mimi, changamoto zinazotusumbua kama taifa kwa sasa ni matokeo ya kutojifunza uzoefu na kuboresha mazuri ambayo yametufanya kudumu miongo sita katika uhuru, amani na umoja uliojengeka kutoka makabila zaidi ya 120 bila ubaguzi wa rangi au tofauti ya ngozi.

Moja ya mambo ya msingi tuliyorithishwa na waasisi wa taifa letu ni wimbo wa taifa. Vijana wengi wa kizazi kipya hawajui hata kuuimba, na pengine huona ni sehemu tu ya itifaki isiyokuwa na umuhimu mkubwa au wa pekee.

Ninapenda kuchukua nafasi hii ya leo kama fursa ya pekee ya kueleza imani yangu kuhusu umuhimu na maana kubwa ya wimbo wa taifa ambao tumerithishwa na waasisi wa taifa kama tunu yenye thamani kubwa sana.

Wimbo wa Taifa wa Tanzania ni dua yenye sehemu mbili. Kwanza ni kumuomba Mwenyezi Mungu abariki Afrika yote bila ubaguzi, na Tanzania ikiwemo.

Walengwa wa kipekee katika sehemu ya kwanza ya dua hiyo ni viongozi. Haibagui viongozi wa ngazi gani wala maeneo ya uongozi; dini, siasa, serikali, uchumi, jamii, majeshi au kundi lolote la Afrika linaloongozwa.

Maombi kwa Mwenyezi Mungu kupitia wimbo wa taifa ni kujaliwa viongozi watakaotekeleza majukumu ya dhamana ya uongozi kwa: Kufundishwa kuongoza kwa kutumia hekima; kujenga, kustawisha na kuimarisha umoja; kujenga, kustawisha na kudumisha amani.

Sehemu ya pili ya dua inajielekeza kuiombea kipekee Tanzania. Walengwa ni Watanzania; wake, waume na watoto. Baraka za Mwenyezi Mungu zidumishe uhuru wa Tanzania; umoja wa taifa letu la Tanzania.

Kwa hiyo, kwa kuongozwa na maudhui ya dua hiyo ya Watanzania wote bila ubaguzi wa aina yoyote, binafsi nimejipatia jicho, darubini, sikio na kigezo cha chama, kikundi au yeyote anayeandika, anayejionesha au anayesimama hadharani na kusema chochote kuhusu Tanzania, humpima kwa kujiuliza bila kudhania:

“Huyu anaishi, anaongea au anatenda kwa kuongozwa na misingi ya hekima? Anajenga au anaimarisha na kustawisha umoja wa Tanzania? Huyu anajenga na kustawisha pamoja na kuilinda amani ya Tanzania? Huyu anatenda na anajipambanua kama mlinzi wa kutetea, kulinda na kudumisha uhuru wa nchi yetu?”

Kwa kutumia misingi ambayo waasisi wa taifa waliheshimu na kuienzi kiasi cha kumuomba Mwenyezi Mungu katika dua ya pamoja, nimepata namna ya kusikiliza, kuchambua na hatimaye kupata msimamo thabiti wa masuala yanayohusu tathmini ya hali iliyopo na mustakabali pamoja na mwelekeo wa yale yajayo.

Ujumbe ni kwamba yapo mambo ya msingi ambayo tumerithishwa na tukiyathamini yanaweza kusaidia taifa, lakini kuna hatari kubwa ya kupuuzwa au kutelekezwa kwa hasara kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Hali hiyo inaweza kusababishwa na tabia ya kuiga tamaduni na mitazamo ya nchi za nje, hususani Marekani na Ulaya, kwa kuamini dhana kwamba dunia ni kama kijiji.

Ni kweli kwamba dunia ya leo ni ya kutegemeana, ya muunganiko na ya mitandao inayosomana kwa sababu ya mapinduzi na maendeleo katika biashara, usafiri na usafirishaji pamoja na utalii.

Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kwamba uhalisia wa matendo ya nchi za Marekani na Ulaya wakati mwingine ni kinyume na mwelekeo wa maendeleo ya ulimwengu wa sasa.

Hoja yangu ni kwamba tukitaka kudumu katika hali ya usalama, hatuna budi kuendelea kusimamia misingi iliyotuletea uhuru, umoja na amani kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.

Ninakubaliana kwa asilimia 100 na maoni kwamba msingi wa amani ni haki, na haki hupatikana kama matokeo ya muunganiko wa haki jamii na haki uchumi.

Falsafa na itikadi ya ujamaa na kujitegemea zililenga hayo mawili ili kuweka misingi ya sera za kufikia malengo ya kupigania uhuru. Haiwezekani kujitegemea bila kujenga uchumi wa viwanda.

Ndiyo maana tulipigwa vita sana hadi wengi miongoni mwetu wakakata tamaa, wakasalimu amri na kukengeuka katika fikra, falsafa na maono kuhusu mustakabali na maendeleo ya jamii ya Watanzania.

Kwa mtazamo wangu, sishawishiki kukubaliana na maoni yanayoendelea katika mijadala ya mabadiliko ya katiba na sheria kwamba ndiyo masuala ya msingi yanayohitaji kipaumbele kwa sasa.

Mtazamo wangu huo unatokana na kujifunza kutokana na uhalisia wa mambo duniani, nje na ndani ya Tanzania.

Tujiangalize kwanza nje, ambako kuna mvuto mkubwa wa kuiga kwa sababu ‘wenzetu’ wameendelea kiuchumi na kiteknolojia. Tangu miaka ya 90 hadi sasa, Marekani imeongozwa na marais tofauti kwa katiba ile ile bila mabadiliko makubwa.

Aidha, katika zaidi ya miaka 200, Marekani imeendelea kutumia katiba ile ile yenye marekebisho kadhaa yaliyofanyika kwa nyakati tofauti.

Ukweli mwingine ni kwamba Uingereza haina katiba iliyoandikwa, lakini ina mfumo imara wa maadili unaoongoza utawala wake.

Mifano hii inaonesha kuwa maadili yana nafasi kubwa kuliko hata sheria katika kujenga utawala bora.

Jirani zetu Kenya wana katiba mpya, lakini changamoto zinazoonekana zinahusiana zaidi na masuala ya maadili katika siasa.

Hata tukitazama China na India, tunaona kuwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii hayategemei tu aina ya mfumo wa kisiasa bali pia maadili ya uongozi.

Maadili ndiyo yanayoleta tofauti ya mwenendo na matokeo ya kila awamu ya uongozi katika nchi yoyote, ikiwemo Tanzania.

Kwa hiyo, ninashauri Watanzania tujihoji na kujitathmini kuhusu namna ya kuhakikisha uendelevu wa uongozi bora kwa kuimarisha taasisi za malezi ya uzalendo, hususani Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Lengo ni kujenga mfumo imara wa kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora katika ngazi zote za jamii—kuanzia familia hadi serikali na taasisi mbalimbali.

Ninatumaini wapo watakaokubaliana na hoja kwamba changamoto ya msingi kuhusu mwenendo wa sasa na mustakabali wa Tanzania ni suala la maadili.

Habari Zifananazo

3 Comments

  1. Immediate cashout options can add a strong sense of ccomfort tto the overall online gaming experience.
    With a gaming site focused on rapid cashout access, players can move from gameplay to
    cashout with greater ease. Such a smooth withdrawal setup often creates a more relaxed atmosphere.
    A lot of plyers value simple cashout instructions,
    modern financial tools, and a comfortable platform structure.
    Together, these elements support a pleasant environment that feels easy to manage throughout play.

  2. Awesome post! I have been interested in vehicle reviews laztely and this article gave me fresh
    ideas. Really enjoyyed the route suggestions. Will definitely come back for more.
    Thank you for sharing your knowledge. More
    like this please!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button