NEMC yatoa maagizo saba kukabili mvua za El Niño

DAR ES SALAAM: Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa maagizo saba ya haraka kwa wananchi na taasisi nchini ili kuzuia mvua za El Niño kusababisha mafuriko, vifo na uharibifu wa mali unaoweza kuepukika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma wa NEMC, Martha Kawishe, amesema wananchi wanapaswa kuhakikisha mifereji, makalavati na njia za maji zinakuwa safi kwa kuondoa taka na vitu vingine vinavyoweza kuziba mtiririko wa maji.
Aidha, Meneja huyo amesema wananchi wanapaswa pia kuacha kutupa taka ovyo, hususan kwenye mifereji, njia za maji na maeneo mengine yanayoweza kuzuia mtiririko wa maji na kuongeza hatari ya mafuriko.
Akisisitiza juu ya utunzaji wa mazingira kuepuka athari za mvua hizo, Kawishe amewataka wananchi kulinda kingo za mito, mabonde na maeneo oevu, na kuepuka shughuli zinazoweza kuharibu maeneo hayo nyeti kimazingira.
“Mvua ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Taifa kwa kuwa zinawezesha kilimo, uvuvi, upatikanaji wa maji na uzalishaji wa umeme. Hata hivyo, matumizi yasiyofaa ya ardhi na uharibifu wa mazingira vinaweza kusababisha madhara makubwa wakati wa msimu wa mvua,” alisema.
Pia, Baraza hilo limewataka wananchi kuchukua tahadhari zaidi katika maeneo yanayokabiliwa na mafuriko, yakiwemo miteremko, maeneo ya milimani, mabonde, njia za maji na maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu na shughuli za kiuchumi.
“Tunawaasa wananchi wanaofanya shughuli za kilimo kwenye kingo za mito, karibu na vyanzo vya maji na mabondeni kuhamia maeneo salama ili kulinda maisha yao na mazingira,” alisema meneja huyo.
Hata hivyo, baraza hilo liliagiza viwanda, hospitali, migodi, karakana na maeneo ya kuhifadhi mafuta na kemikali hatarishi kuhakikisha kemikali na mafuta vinahifadhiwa katika mazingira salama ikisema kwamba biashara au hifadhi isiyo salama ya kemikali na mafuta inaweza kusababisha vitu hivyo kusombwa na maji wakati wa mvua kubwa na kuchafua vyanzo vya maji, jambo linaloweza kuhatarisha afya za binadamu, wanyama, mifumo ya ikolojia na bioanuwai.
“Lakini pia, tunawataka wasimamizi na waendelezaji wa miradi kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za mazingira kabla na wakati wa utekelezaji wa miradi yao,” alisema.
Kwa upande wao, mamlaka za Serikali za Mitaa zimetakiwa kuendelea na majukumu yao ya kawaida, ikiwamo kutoa elimu kwa umma na kubaini maeneo hatarishi kwa mafuriko ili hatua za kuzuia mafuriko zichukuliwe mapema.
Aidha, Kawishe alisema uhifadhi wa mazingira si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa pamoja wa wananchi, wafanyabiashara, taasisi na wadau wengine.
Alisema NEMC itaendelea kufuatilia uzingatiaji wa sheria za mazingira katika miradi ya maendeleo, masoko, viwanda na maeneo mengine, na kuchukua hatua za kisheria pale itakapobaini ukiukwaji.



