NHIF yahamasisha kujiunga bima kupunguza gharama za matibabu

DODOMA: MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeendelea kuhamasisha wananchi kuacha kutegemea malipo ya papo kwa papo wanapohitaji matibabu na badala yake kujiunga na Bima ya Afya ili kujikinga na gharama kubwa za huduma za afya na kupata matibabu kwa urahisi katika vituo vya serikali, binafsi na taasisi za dini vilivyosajiliwa na mfuko huo.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Masoko na Huduma kwa Wateja wa NHIF, Angellah Mziray, wakati wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma, ambapo alisema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kuwafikia wakulima na makundi mbalimbali ya wananchi kwa kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya.

Mziray alisema kujiunga na bima ya afya kunawawezesha wananchi kupata kinga dhidi ya gharama zisizotarajiwa za matibabu, badala ya kusubiri kuugua na kulazimika kuuza mali au kutumia fedha nyingi kugharamia huduma za afya.

Alisema kuwa serikali imeweka utaratibu unaomwezesha mwananchi kuchangia kidogo kidogo ili kuhakikisha anapata huduma za matibabu pale zinapohitajika, hatua inayochangia kulinda ustawi wa familia na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji.

Alisema ushiriki wa NHIF katika Maonesho ya Nanenane unalenga kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ambayo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na ulinzi wa bima ya afya.

“Afya ni msingi wa maendeleo ya familia na uchumi wa taifa. Tunawahimiza wananchi, hususan wakulima, kutumia fursa ya maonesho haya kujiunga na NHIF ili wawe na uhakika wa kupata huduma za afya bila kubeba mzigo mkubwa wa gharama za matibabu.”

Mziray aliongeza kuwa uwekezaji katika bima ya afya unawapa wananchi nafasi ya kuelekeza rasilimali zao katika shughuli za maendeleo badala ya kutumia fedha nyingi kukabiliana na matibabu ya dharura, huku akisisitiza kaulimbiu ya mfuko huo ya “Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa” kuwa ndiyo njia sahihi ya kujenga jamii yenye afya, ustawi na nguvu kazi yenye tija kwa maendeleo ya taifa

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button