Pangani watangaza fursa zao la popoo

MOROGORO; Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Seif Ally amesema zao la popoo linalolimwa Pangani, mkoani Tanga lina fursa kubwa kiuchumi.
Akizungumza alipotembelea bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa Wilaya ya Pangani kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mjini Morogoro, mwenyekiti huyo alisisitiza umuhimu wa wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo.

Seif aliyeambatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Whitney Mwizagi, amesema zao la popoo linalolimwa Wilaya ya Pangani, ni miongoni mwa mazao yenye fursa kubwa kiuchumi kwa wakulima endapo litaendelezwa kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo, uvunaji na uongezaji thamani.
Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima, wajasiriamali na halmashauri ili kuhakikisha mazao yanayolimwa Pangani yanapata soko la uhakika na yanatumika kuongeza kipato cha wananchi.



