Rais aitaka jamii iache ubinafsi, ifikirie vizazi vijavyo

RAIS Samia Suluhu Hassan ameitaka jamii kuyaishi kwa vitendo maneno ya Mwenyezi Mungu kwa kuacha tabia ya ubinafsi na kuvifikiria vizazi vijavyo.
Ametoa mwito huo jana jijini Tanga wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi na upanuzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa.
Rais Samia alisema kuna watu wengi wenye uwezo wa kuwasaidia ndugu zao wa damu pamoja na kutekeleza miradi mingi ya kimaendeleo kwa ajili ya jamii iliyopo na vizazi vijana, lakini kutokana na ubinafsi waliokuwa nao hawafanyi hivyo.
Alisema watu hao huangalia maisha yao ya sasa bila ya kujali maisha ya watu wengine na maisha yao baada ya kifo.
“Tujiulize ni wangapi wanakwamisha miradi mikubwa ya maendeleo, tena miradi inayowanufaisha hata wao wenyewe kwa uchoyo tu wa nafsi zetu?” alihoji.
“Ni wangapi wanashikilia maeneo makubwa ya ardhi ambayo hawayaendelezi lakini hawayaachii kwa walio tayari kuyaendeleza achia mbali kuyatoa wakfu”.
Alisema kitu alichofanya marehemu Sharif Haidar bin Ahmed cha kutoa kipande chake cha ardhi kwa ujenzi wa msikiti ambao unakwenda kupanuliwa kwa udhamini wa Kampuni ya Lake, ni mfano bora wa mtu mwenye imani ya kweli kwa dini yake.
Alisema Sharif Haidar bin Ahmed ametoa kipande cha ardhi kujenga msikiti katika mji mashuhuri, kitu ambacho ni kigumu kwa wengine kutokana na uthamani wa ardhi.

“Watu wanapigana na kuuana kwa sababu ya ardhi, ndugu wanagombana kisa ardhi, majirani hawasemeshani kisa wameingiliana katika ardhi, mataifa yanaingia vitani tunasikia huko Congo… tunapigana kwa sababu ya ardhi, lakini mzee wetu huyu aliona atoe wakfu sehemu ya ardhi yake aliyoimiliki,” alisema Rais Samia.
Vilevile, Rais Samia alisema taasisi za dini zina jukumu kubwa la kulinda na kukuza maadili, na alizitaka kuungana katika kulinda maadili ikiwamo kukomesha biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema serikali ina mipango mingi ya maendeleo kwa ajili ya Mkoa wa Tanga na kubainisha kuwa mipango hiyo itakuwa haina tija kama vijana watakuwa wameangamia na matumizi ya dawa za kulevya.
Aliishukuru Kampuni ya Lake kwa kurudisha kwa jamii kupitia sekta ya afya, elimu pamoja na ujenzi na upanuzi wa msikiti huo unaogharimu Sh bilioni sita.
“Bilioni sita ni fedha nyingi sana, mimi serikalini ukiniambnia ninakupa bilioni sita sasa hivi nimeshajenga hospitali ya mkoa kama sio ya wilaya na vifaa vyake vyote,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alisema amepokea ombi la ujenzi wa uzio katika eneo la makaburi ya Msambweni na kuahidi kulifanyia kazi.



