Shule ya msingi Makangaga yapata darasa jipya

LINDI: SHULE ya Msingi Makangaga iliyopo Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi imepokea darasa jipya kutoka katika kampuni ya uzalishaji bidhaa za ujenzi Knauf Gypsum ikiwa ni hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuchangia maendeleo ya jamii.
Akizungumza jana wakati wa makabidhiano hayo Mkuu wa Shule ya Makangaga,Mwalimu Frank Theobald amesema darasa hilo litasaidia kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa na kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi.
Amesema uwepo wa darasa hilo utasaidia kupunguza utoro na kuwawezesha wanafunzi kufikia malengo yao ya kitaaluma.
“Jengo hili jipya litasaidia kupunguza upungufu wa madarasa, kupunguza utoro wa wanafunzi na kuwawezesha kufikia malengo yao ya kitaaluma,”amesema Mwalimu Theobald.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Makangaga, Seleman Mnonya amesema darasa hilo ni sehemu ya mchango ambao Knauf imekuwa ikitoa kwa jamii, ikiwamo madawati, kisima na misaada mingine kwa ajili ya mahitaji ya wananchi.
Amesema jamii ina matumaini ya kuendelea kunufaika na miradi mingine ya maendeleo kutoka kampuni hiyo.
Naye Meneja wa Sheria, Mahusiano ya Nje na Serikali wa Knauf Gypsum,Frola Erasto amesema kukabidhiwa kwa darasa hilo ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kuchangia maendeleo ya jamii.
“Tunafurahi kukabidhi darasa hili jipya kwa shule ya Msingi Makangaga kama sehemu ya dhamira yetu ya kuendelea kuboresha jamii. Hapo awali tumetoa madawati, viti, kisima na misaada mingine kwa kijiji hiki, lakini hatupimi kile tunachofanya, kwa sababu huu ni wajibu wa Knauf,”amesema Erasto.

Kwa upande wake mwanafunzi wa darasa la sita Nurat Hassan ameeleza kuwa darasa hilo limewaongeze hamasa ya kuongeza bidii katika masomo.
Mwanafunzi mwingine, Daivat Abdallah, aliishukuru Knauf kwa kuwapatia darasa hilo na kueleza kuwa darasa hilo limetawahamasisha kusoma kwa bidii zaidi.



