Tanzania yatoa mchango uanachama EAC asilimia 100

DODOMA; Serikali ya Tanzania imesema tayari imeshatoa mchango wake wa uanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (AEC) kwa mwaka wa fedha 2026/2027

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Ussi Yahya.

Mbunge huyo alihoji serikali imejipangaje kuhakikisha uhai na uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikizingatiwa kuwa malipo ya michango ya nchi wanachama yamekuwa yakisuasua.

“Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu, kuwa Tanzania kama Mwanachama hai na mwaminifu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, tayari imeshatoa mchango wake wa Mwaka huu wa Fedha 2026/2027 kwa asilimia 100,” amesema Naibu Waziri.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kulinda na kutetea maslahi ya Taifa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuhakikisha kuwa, Jumuiya inaendelea kuimarika na kunufaika kupitia utekelezaji wa programu za maendeleo, ukuaji wa biashara, ongezeko la uwekezaji katika miundombinu na huduma za kijamii.

“Pamoja na manufaa yanayopatikana, changamoto kubwa inayoikabili Jumuiya kwa sasa ni michango ya baadhi ya Nchi Wanachama kutotolewa kwa wakati na ukamilifu hali inayoathiri utekelezaji wa shughuli na programu za jumuiya.

“Aidha, Serikali imeendelea kuchukua hatua katika kuhakikisha kuwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki inaendelea kuwa hai na inatekeleza kikamilifu majukumu yake.

“Mathalan, Tanzania ilikuwa sehemu ya maamuzi ya Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika Machi 2026 ambao uliidhinisha mfumo mpya wa uchangiaji ambapo 50% ya mchango utatolewa kwa usawa na kila Nchi Mwanachama na 50% utatokana na uwezo wa uchumi wa nchi husika (GDP). Mfumo huu umeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Julai 2026,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button