Tanzania yatumia teknolojia kukuza uchumi wa buluu

DAR ES SALAAM: SERIKALI imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali, mifumo ya kisasa ya usimamizi wa bandari na biashara, pamoja na matumizi ya taarifa za kisayansi katika kufanya maamuzi kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamadi Masauni, amesema hayo leo Septemba 7, 2026, kwa niaba ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, wakati akihutubia Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu 2026, lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Masauni amesema uchumi wa buluu wa kisasa unahitaji wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu, ubunifu pamoja na uwezo wa kutumia teknolojia mpya, hivyo taasisi za elimu ya juu na utafiti, ikiwemo Dar es Salaam Maritime Institute (DMI), zina nafasi muhimu katika kuzalisha rasilimali watu wenye uwezo wa kuendesha mabadiliko katika sekta hiyo.
Amesema mafanikio ya uchumi wa buluu yanategemea kwa kiasi kikubwa utafiti wa kisayansi na ubunifu, ambao unalenga kuongeza uelewa kuhusu uwezo wa rasilimali zilizopo, kuboresha uzalishaji, kutengeneza bidhaa mpya, kuongeza thamani ya mazao ya bahari na kulinda mazingira.

“Mkutano huu unatukumbusha kuwa mafanikio ya uchumi wa buluu yanategemea utafiti wa kisayansi na ubunifu. Tafiti zitatusaidia kufahamu uwezo wa rasilimali zetu, kuboresha uzalishaji, kutengeneza bidhaa mpya, kuongeza thamani ya mazao na kulinda mazingira yetu,” amesema Masauni.
Aidha, Masauni amezitaka sekta binafsi kutumia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu, ambapo ametaja maeneo ya uwekezaji kuwa ni pamoja na biashara ya kaboni ya bluu, bioteknolojia ya baharini, uongezaji thamani wa mazao ya bahari pamoja na huduma za kilojistiki zinazosaidia maendeleo ya sekta hiyo.
Kwa upande wake, ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria , Neema Mwanga, amesema ushiriki wa wizara hiyo katika kongamano hilo unalenga kuhakikisha masuala yote ya kisheria yanayohusiana na uchumi wa buluu yanasimamiwa ipasavyo.
Mwanga amesema wizara hiyo ina jukumu la kuhakikisha sheria zinakuwa rafiki na wezeshi katika kusimamia shughuli za uchumi wa buluu, ikiwemo matumizi, uvunaji na uwekezaji katika utajiri na mali asili za nchi.
Amesema sheria ambazo zinatoa vikwazo katika kuvuna, kutumia na kuwekeza katika rasilimali za nchi zinaendelea kufanyiwa marekebisho ili kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kuongeza uwezo wa Tanzania kuvutia wawekezaji katika uchumi wa buluu.




