India kuongeza soko la mazao Tanzania

SERIKALI ya India imesema iko katika hatua za kuchunguza fursa za kuongeza kiwango cha bidhaa za kilimo kutoka Tanzania zinazoingia katika soko la India, hatua inayolenga kuongeza mauzo ya nje, kuboresha ubora wa mazao na kukuza ajira nchini.

Hayo yamesemwa leo, Septemba 2, 2026, na Mwakilishi Mkuu wa India nchini Tanzania, Shri Bishwadip Dey, wakati wa Maonesho ya 10 ya Kimataifa ya Kilimo Barani Afrika yaliyofanyika Viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaam.

Dey amesema Tanzania na India zina uhusiano mzuri katika sekta mbalimbali, huku akieleza kuwa kilimo ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za kuongeza ushirikiano, hususan katika uzalishaji, usindikaji, mafunzo na masoko.

Amesema India ni miongoni mwa masoko makubwa ya bidhaa za kilimo kutoka Tanzania, zikiwemo korosho, kunde na parachichi, na kwamba nchi hiyo iko tayari kushirikiana na Tanzania kupitia teknolojia, uzoefu, rasilimali na mafunzo.

“Tunataka kuchunguza fursa za kuongeza kiwango cha bidhaa za Tanzania zinazouzwa nchini India, huku tukiboresha ubora wake, ili kuongeza mauzo ya nje na hatimaye kuongeza fursa za ajira nchini Tanzania,” amesema Dey.

Aidha, Dey ameitaka Tanzania kuendelea kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuimarisha mafunzo kwa wakulima ili kuongeza tija na ubora wa mazao. Amesema maonesho hayo, yaliyoshirikisha zaidi ya kampuni 1,000, yametoa fursa kwa wadau wa kilimo kutoka ndani na nje ya Tanzania kubadilishana uzoefu, kuonesha teknolojia na kutafuta fursa za biashara na uwekezaji.

Dey amewashukuru waandaaji wa maonesho hayo, TAB na TanTrade, akisema jukwaa hilo ni muhimu katika kujenga ushirikiano na kufungua fursa mpya katika sekta ya kilimo.SOMA: Mauzo ya mazao yaongezeka asilimia 43.6

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button