Mwigulu: Watanzania washike uchumi

WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ametoa wito wa kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi kwa kunufaika na fursa za ajira, biashara, uwekezaji na umiliki wa shughuli za kiuchumi. Dk. Mwigulu ameyasema hayo jana, Septemba 3, 2026, jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la Tano la Taifa la Ushiriki wa Watanzania katika Masuala ya Uchumi.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira ya kisera, kisheria na kiutendaji yatakayowawezesha Watanzania kushiriki katika uchumi, akisisitiza kuwa hatua hiyo hailengi kuwazuia wawekezaji wa nje. Hatahivyo ameiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha marekebisho ya sheria za ununuzi yanaongeza wigo wa miradi inayoweza kutekelezwa na kampuni za Kitanzania.
Amesema kiwango cha Sh bilioni 50 kwa baadhi ya miradi kimekuwa kidogo kutokana na kukua kwa uchumi na uwezo wa kampuni za ndani, hivyo kupendekeza kiongezwe hadi zaidi ya Sh bilioni 100 au Sh bilioni 150. SOMA: Songwe yaongoza njia mageuzi ya kiuchumi Dira 2050
Katika hatua nyingine, Dk. Mwigulu amezindua Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Uwezeshaji Kiuchumi (NEMIS), unaolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu fursa za mitaji, zabuni za umma, uwekezaji na programu mbalimbali za uwezeshaji.
Amesema Tanzania ina rasilimali na fursa nyingi za kiuchumi, hivyo ni muhimu kuhakikisha zinageuzwa kuwa ajira, biashara, uwekezaji na umiliki kwa Watanzania. Pia amesisitiza kampuni zinazotekeleza miradi ya Serikali kutumia fedha kwa uadilifu na kutoa huduma kwa kiwango na ubora unaostahili.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema manunuzi ya bidhaa na huduma katika sekta ya madini yanafikia Sh trilioni 5.1 kwa mwaka, huku Serikali ikihakikisha asilimia 90 ya manunuzi hayo yanafanyika nchini ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Serikali imeendelea kuweka sera, sheria na mifumo ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uchumi.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi, Prof. Aurelia Kamuzora, amesema uwezeshaji unapaswa kwenda sambamba na upatikanaji wa mitaji, taarifa, ujuzi na kujenga uwezo wa Watanzania ili waweze kushindana ndani na nje ya nchi.



