MWENYEKITI wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA TAN), Wakili James Marenga amesema kuwa mabadiliko ya sheria yeyote hapa nchini huwa yanachukua muda mrefu.
Amesema kuwa wakati mzuri ni sasa wa kufanya mabadiliko ya sheria za habari kwa kuwa, serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeonesha dhamira hiyo.
Marenga ameyasema hayo wakati akizungumza katika Kituo cha Redio Tumaini jijini Dar es Salaam, kuhusu mwanya uliopo kwenye sheria za habari na hatari yake.
“Mchakato wa marekebisho ya sheria iliyotungwa mwaka 2016, ulichukua miaka 10. Mchakato huo ulianza mwaka 2006, ni bahati utawala uliopo umeona kuna haja ya kupitia upya sheria hizi kama ambavyo wadau wamekuwa wakipiga kelele.
“Tunaamini sheria hizi na zingine ambazo tumeorodhesha kwenye nakala yetu ya mapendekezo ya mabadiliko, wadau na serikali kwa pamoja tutapitia na kuona namna ya kunyoosha, ili mapendekezo hayo yatapopelekwa bungeni, tuwe na msimamo unaofanana,” amesema Marenga.