‘Tunafanya kazi kisheria’

MWENYEKITI wa Maafisa wa Uokoaji (Beach Boys), Almasi Masiya, amekanusha madai kwamba baadhi ya watoa huduma hao huwafanyia vitendo visivyofaa wanawake wanaokwenda kujifunza kuogelea akisema kazi yao kubwa ni kuwafundisha kuogelea na kuhakikisha usalama wao wanapokuwa majini.
Masiya aliyasema hayo wakati akizungumza na Daily News Digital katika ufukwe wa Coco Beach, jijini Dar es Salaam. Amesema maafisa wa uokoaji wanaofanya shughuli hiyo husajiliwa na mamlaka zinazohusika na usajili wa vikundi na taasisi, huku akieleza kuwa kazi zao zinahusisha kuwafundisha watu kuogelea na kutoa huduma za uokoaji.
Kwa mujibu wa Masiya, baadhi ya watu wanaohusishwa na vitendo visivyofaa katika maeneo ya ufukwe si Beach Boys halisi, bali ni watu wanaojitambulisha kwa jina hilo bila kuwa na uhusiano na kundi hilo. “Kuna watu ambao wanakuja beach ambao sio Beach Boys, lakini wanakuwa na kimo na umri wa vijana wa Beach Boys. Hujifanya ni Beach Boys na kuwachukua wanaohitaji kuogelea na kwenda kuwafanyia vitendo vibaya,” alisema.
Kwa upande wake, mjasiriamali wa Coco Beach, Festo Elias amesema eneo hilo linatembelewa na watu wengi na ni sehemu ambayo wananchi wanaweza kwenda kwa ajili ya mapumziko na kuogelea. Pia amekanusha kuwepo kwa malalamiko yanayohusisha Beach Boys na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake wanaokwenda kuogelea.
“Habari za Beach Boys kuwafanyia vitendo vibaya wanawake sio za kweli. Hata ukienda kituo kidogo cha polisi jamii kilichopo maeneo ya Coco Beach, hawana malalamiko yoyote yanayohusiana na Beach Boys kuwafanyia vitendo vibaya watu wengine,” alisema.

Naye William James anayehusika na ulinzi wa waogeleaji (lifeguard) amesema usalama wa watu wanaokwenda kuogelea unahitaji uwepo wa watu wenye ujuzi pamoja na vifaa sahihi vya uokoaji. Alisema hali ya uchafuzi katika eneo hilo imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kipindi cha nyuma. Mteja wa Coco Beach, Margreth Sai, alisema kuwepo kwa utambulisho rasmi na usimamizi mzuri wa Beach Boys kunaweza kuongeza usalama kwa watu wanaokwenda kujifunza kuogelea. SOMA: Mtanzania ang’ara kuogelea baharini Kenya
“Kwenda kwa watoto wa kike ufukweni ni jambo zuri iwapo wanaenda na mtu wa kuwasimamia. Beach Boys ni muhimu sana katika maeneo haya kwa sababu wanasaidia watoto na watu wazima ambao hawajui kuogelea na wanataka kujifunza. Cha muhimu ni kuwepo kwa utambulisho wa Beach Boys ili iwe rahisi kuwafahamu,” alisema. Hata hivyo, mwimbaji Gold Ndilivale, anayejitafutia kipato kupitia muziki, alisema hakuna mtu anayeweza kumpeleka mwanamke majini na kumfanyia vitendo visivyofaa bila mwanamke huyo kuonyesha dalili za kutaka jambo hilo.
Amesema wanawake wanaokwenda ufukweni kwa lengo la kujifunza kuogelea hawafanyiwi vitendo vya ukatili na Beach Boys, akidai kuwa baadhi ya wanaume wanaojitambulisha kama waokoaji wanaweza kuwa watu wasiohusika na kundi hilo. “Wanawake wanaokuja kwa lengo la kuogelea huwa hawafanyiwi ukatili na Beach Boys, ila kuna wanawake wanaokuja na kuwaomba vijana ambao sio Beach Boys wawasaidie vifaa vya kuogelea au kuwafundisha kuogelea. Hali hiyo inaweza kumfanya mtu kutamani kufanya kitendo ambacho si kizuri,” alisema.



