Waandishi, wananchi wafundwa mabadiliko tabianchi

WAANDISHI wa habari na wananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini wamefundwa athari za mabadiliko ya tabia ya nchi na namna ya kuripoti kwa usahihi ili makundi yanayoathirika yapatiwe msaada.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Shirika la Women Action Towards Economic Development (Wated) ambapo yameshirikisha wananchi wa mikoa mitano ya Kagera, Lindi, Mtwara, Manyara na Dar es Salaam sambamba na waandishi wa habari.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika Dar es Salaam Mratibu wa Wated Maria Matui amesema mabadiliko ya tabia nchi yanapotokea kwa mfano ya ukame, mafuriko na njaa waathirika wakubwa ni wanawake na watoto.
Amesema kuna haja ya serikali kuangalia uwezekano wa kusaidia makundi ya wanawake hasa katika maeneo yanayoathirika kwa kuwa asilimia kubwa hufanya shughuli za kilimo hasa chakula na mazingira huwahusu.
“Tunatamani kuona dhana ya kupata rasilimali fedha iwafikie wanawake hasa wa maeneo ya vijijini washiriki katika mapambano ya tabia nchi,
“Taarifa sahihi za mabadiliko ya tabia nchi ziwafikie pia. Na matumizi ya nishati safi waangaliwe kwa gharama watakazomudu kwa kuwa ndio waathirika,”amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha usuluhishi (CRC) chini Chama cha Wanawake Wanahabari Tanzania Gladness Munuo amesema waandishi wa habari wanapaswa kufahamu mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kijinsia.
“Tunafahamu kabisa ukitaja mazingira au tabia nchi tunamgusa mwanamke moja kwa moja, tunajua ndiye anayeshughulika na ukulima mdogo mdogo wa chakula, hutafuta maji ndani ya nyumba, kutafuta nishati,”
“Waandishi wa habari watoe elimu kwa watunga sera kwamba hii nishati safi tunayotaka mwanamke au mtanzania kama anaipata kwa urahisi au ngumu, watunga sera wakisikia wachukue maamuzi,”amesema.
Mwisho



