Wadau walalamikia Kigoma kubadili matumizi maeneo wazi

Wenyeviti vijiji waliouza ardhi kiholela matatani

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imelalamikiwa kwa kubadili matumizi ya awali ya maeneo ya wazi na yaliyotengwa kwa ajili ya huduma za jamii na kugeuza makazi.

Imeelezwa kuwa mpango wake inaotekeleza sasa wa kupima na kuuza maeneo ya wazi na yale yaliyotengwa kwa ajili ya huduma za jamii yatakuja kutiaa hasara halmashauri hiyo itakapokuwa na miradi ya ujenzi ya huduma za jamii.

Meya Mstaafu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hussein Ruhava akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma ameitaka halmashauri hiyo kuacha mara moja utekelezaji wa mpango huo kwani hauna afya kwa maendeleo ya halmashauri na mji wa Kigoma.

Advertisement

Ruhava alisema halmashauri imebaini uwepo wa maeneo ya wazi 46 ambayo yamejadiliwa kwenye kikao cha mipango miji cha Januari 13 mwaka huu na kuridhiwa na baraza la madiwani Mei 13 mwaka huu, ambapo wamekubaliana kupima na kuuza maeneo hayo yakiwemo maeneo maalumu ya uhifadhi wa mazingira.

“Mpango huu unaenda kinyume na mpango mkakati wa halmashauri uliopitishwa mwaka 2017 ambao unayatambua maeneo hayo kama maeneo ya wazi ambayo yanapaswa kutumiwa kwa ajili ya miradi ya umma lakini kulindwa na kutunza kwa ajili ya shughuli za pamoja na siyo kuuzwa kwa ajili ya ujenzi wa makazi,” alisema.

Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji katika baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa mwaka 2015 hadi 2020, Hussein Kalyango alisema kupinga kwao kutekelezwa kwa mpango ni namna ambavyo madiwani wameamua kwa pamoja kuungana kutekeleza mpango ambao hauna maslahi kwa mji wa Kigoma Ujiji.

Kalyango alisema zipo athari kubwa za kukosa maeneo hayo kwa halmashauri lakini aliongeza kuwa nyuma ya pazia ya mpango huo ni hatua ya madiwani ya kutaka kujigawia maeneo hayo na baadaye kuyauza kwa watu wengine.

Alisema mapendekezo ya kamati ya mipango miji na baraza la madiwani ni kuyapima na kuyauza maeneo hayo kwa bei ya soko ya mita za mraba tofauti na thamani halisi ya eneo lilipo na hiyo ndiyo sababu ya hofu ya kutaka kuzuia mpango huo.

Akitoa maazimio ya mpango huo, Frank Ruhasha mmoja wa wananchi wanaopinga mpango huo alisema baada ya mkutano huo na waandishi wa habari wanatarajia kupeleka barua kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Tamisemi, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (LAAC).

Lakini pia kuitisha mikutano ya wananchi kata zote za manispaa ili kuwaeleza uhalisia na kuwaomba kuwaunga mkono katika kupinga mpango huo.

Akijibu tuhuma na malalamiko hayo Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji aliye madarakani, Baraka Lupoli alikiri kuwepo kwa mpango wa kupima na kuuza maeneo ya wazi 46 ambaye yametambuliwa baada ya kufanya ziara kutembelea na kuyaainisha.

Lupoli alisema mpango huo unalenga kuondoa migogoro inayojitokeza mara kwa mara ambapo wananchi wamekuwa wakivamia na kusema ni maeneo yao ya asili na kwamba badala ya kuwa na migogoro au kuyakosa kabisa ni vizuri halmashauri iuze na kuingiza mapato.

 

 

/* */