Wananchi Kilosa waondokana na shida maji safi

MOROGORO: WAKAZI 6,000 wa kijiji cha Ulaya Kibaoni Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji safi na salama baada ya kukamilika ujenzi wa mradi wa usambazaji maji uliogharimu Sh milioni 174. 3 zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania .
Ofisa wa Wakala wa Maji Safi na Mazingira Vijijini (RUWASA), Getruda Aloyce amesema hayo katika taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi.
Getruda amesema kuwa ujenzi wa mradi huo ulianza Aprili 2024 na kukamilika Julai 2024 na kwamba ulilenga kuwanufaisha wakazi 5,945 wa kijiji cha Ulaya Kibaoni.
Amesema kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa tanki kuu la maji lenye ujazo wa lita 50,0000 juu ya mnara wa mita sita ikiwa na miundombinu ya kitibu maji na ujenzi wa vituo vitano wa kuchota maji .
Getruda amesema ujenzi mwingine ni uzio wa nyumba ya mtambo na ufungaji wa mfumo wa umeme juu kwenye chanzo cha maji.

“ Mradi unalenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hili hususan wanawake na watoto ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji” amesema Getruda.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa wa mwaka huu , Ussi baada ya kukagua na kupokea taarifa ya mradi huo,ameeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea upkuwaletea wananchi wa Kilosa miradi ya maendeleo .
“ Wananachi wa Kilosa hasa wa kijiji hiki ni umuhimu kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo endelevu” amesema Ussi.

Naye Naibu waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki Afrika na Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Dennis Londo amesema wananchi wa vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Kilosa kikiwemo cha Ulaya Kibaoni wamenufaika na upatikanaji wa huduma za maji safi na salama
Mbali na miradi ya maji, amesema katika Kijiji cha Mhenda kwa mara ya kwanza imepata shule ya Sekondari na kwa mara ya kwanza katika historia ya Jimbo la Mikumi inajengewa shule ya kidato cha tano na sita kata ya Ulaya.
Naibu Waziri amesema licha ya ujenzi wa shule katika kata hiyo pia imepatiwa Kituo cha Afya kisasa pamoja na gari la kuhudumia kubeba wagonjwa kwenye tarafa ya Ulaya na vijiji vyake.
Nao baadhi ya Kijiji cha Ulaya Kibaoni wameeleza furaha yao kwa ujio wa Mwenge wa Uhuru na uwepo wa miradi hiyo ya maendeleo hususani upatikanaji wa maji safi na huduma bora za afya utaboresha maisha yao na kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Wakazi hao Ashura Simba pamoja na Jovitha Victory kwa nyakati tofauti wamesema Rais Samia ametumiza ndoto ya wanawake wa kijiji hicho ya kuwatua ndoo kichwani imetimia.
“ Tulikuwa tunakesha kusaka maji mbali , kupatokanaji wa maji hawa umepunguza magonjwa ya kuambukiza kwakuwa watu walikuwa wanachota maji mtoni yasiyosalama “ amesem Ashura.
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo ulikagua miradi ya mandeleo saba yenye jumla ya Sh bilioni 1.8 ambapo Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni “Jitokeze kushiriki uchaguzi wa mwaka huu 2025 kwa amani na utulivu”.



