MKOA wa Mara umeshika nafasi ya tano kitaifa kwa kuwa na wanafunzi wanaohitimu darasa la saba, bila kujua kusoma na kuandika.
Ofisa Elimu wa mkoa huo, Benjamin Oganga, amesema hayo mbele ya viongozi wa elimu wa kada na ngazi tofauti, wa wilaya na mkoa muda mfupi kabla ya uzinduzi wa mkakati wa kitaifa wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu msingi.
Oganga aliyekaimu nafasi ya Katibu Tawala (RAC) wa mkoa huo kwenye kikao hicho leo, Septemba 9 , 2022, amesema mkakati huo uliyozinduliwa kimkoa na Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Suleiman Mzee, utakuwa muarobaini wa changamoto hiyo na nyingine, zikiwamo zinazotokana na mafanikio katika sekta ya elimu.
Changamoto nyingine aliyoitaja ni mdondoko wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.
“Ufatiliaji uliofanywa unaonesha ndani ya miaka mitano, wanafunzi 350,000 katika mkoa huu hawakuhitimu elimu ya msingi kwetu,” amesema Oganga.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Meja Jenerali Mzee ameagiza viongozi wa elimu kuanzia ngazi ya shule mpaka mkoa kushirikiana na mamlaka nyingine, kutafuta kila mwanafunzi aliyetakuwa kuwa shuleni, lakini hayupo na kwamba ikiwezekana wazazi wa wanafunzi hao wabanwe.
“Ili mkakati huu ufanikiwe lazima viongozi mnaosimamia walimu muwe na ubunifu, ili walimu waupokee na kuuzingatia wanapofundisha na kulea watoto wetu,” amesema RC huyo.
Hatahivyo amesema hataki kusikia kiongozi yeyote akitukana wala kugombeza mwalimu mbele ya walimu wenzake, au wanafunzi, kwani hilo linaweza kusababisha mwalimu husika akise kujiamini na hata kuchukia kazi yake.
Ameshauri mbinu za kishawishi zibuniwe na kutumika zaidi badala ya zenye vitisho na kukatishana tamaa.