Waziri wa Ardhi atoa maagizo majengo, vituo vya mafuta

Waziri Dk Angelina Mabula

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula ameagiza kusimamishwa kwa ujenzi wa majengo yanayojengwa kinyume cha sheria nchini.

Dk Mabula pia ametaka kuondolewa kwa vituo vya mafuta ambavyo vimejengwa kinyume cha sheria na kubadilishwa kwa shiria ya umbali wa kituo kimoja cha mafuta hadi kingine kutoka mita 200 za sasa hadi kufikia mita 500.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na makamishina wasaidizi wa ardhi kutoka mikoa mbalimbali, aliagiza kuwa makamishna wa wizara waliotoa hati bila utaratibu kuchukuliwa hatua.

Advertisement

“Tumeendelea kushuhudia ongezeko la ujenzi holela na viongozi wapo na miji inazidi kuharibuka, majengo yanajengwa, lakini hayapo kwenye masterplan, mkasimamie hilo, majengo yanayojengwa kinyume na taratibu yasimamishwe haraka,” amesisitiza.

“Kumezuka vituo vya mafuta kila kona, ilikuwa mita 200 badilisheni iwe mita 500, ikitokea moto umewaka ni hatari sasa vinajengwa kila sehemu bila uthibiti na nyie mnaangalia,” amesema