SERIKALI ya Uganda imetangaza kuiondoa kesi dhidi ya mpinzani, Kizza Besigye kutoka mahakama ya kijeshi na kuihamisha kesi hiyo kwenye mahakama ya kiraia.
Hatua hiyo imetokana na maamuzi kutoka Mahakama ya Juu ambayo yamedai kuwa raia wa kawaida hawezi kufikishwa katika mahakama ya kijeshi, huku pia ikimtaka asitishe mgomo wa kula gerezani.
Soma zaidi: Kiongozi wa upinzani Kizza Besigye akimbizwa hospitali
Besigye, ambaye ni mshirika wa zamani wa Rais Yoweri Museveni na mpinzani wake wa muda mrefu, alianzisha mgomo wa kula Februari 10, 2025 akipinga kifungo chake, ambapo alikamatwa kwa tuhuma za uhaini na madai ya kutishia usalama wa taifa, hatua ambayo ilipingwa na wakosoaji wengi wakiwemo wanasheria na wanaharakati.
Waziri wa Habari, Chris Baryomunsi amesema kuwa alimtembelea Besigye gerezani Jumapili na kumshauri aanze kula ili aendelee kuwa na afya njema wakati akingojea uhamishaji wa kesi yake.
Soma zaidi: Besigye afikishwa mahakama ya jeshi
Kwa upande wake, Mke wa Besigye, Winnie Byanyima, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UNAIDS ameikosoa ahadi ya serikali huku akisema kuwa ni “inatia mashaka” na haionekani kama utawala wa Museveni utatekeleza ahadi hiyo kwa dhati.