Kiongozi wa upinzani Kizza Besigye akimbizwa hospitali

UGANDA : WAFUASI wa kiongozi wa muda mrefu wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, wamefichua kuwa mwanasiasa huyo alikimbizwa hospitalini jana huko Bugolobi.

Kupitia mtandao wa kijamii wa X, mbunge wa Buhweju, Francis Mwijukye, alieleza kuwa Besigye alikimbizwa hospitali akiwa anatumia kiti cha magurudumu, na hospitali hiyo iko katika jengo la kibiashara linaloitwa Bugolobi Village Mall.

Habari hizi zinajiri baada ya familia ya Besigye kuibua wasiwasi kufuatia kupokea ujumbe kutoka idara ya magereza ya Uganda, ikiitaka familia hiyo itume daktari binafsi kwa Besigye.

Advertisement

Besigye alikuwa amewekwa gerezani baada ya kusomewa mashtaka ya kumiliki silaha katika mahakama ya kijeshi ya Uganda.

Mwanasiasa huyu, ambaye alikua daktari binafsi wa Rais Museveni, alikamatwa kwa mazingira ya kutatanisha mwezi Novemba mwaka jana jijini Nairobi pamoja na msaidizi wake wa kisiasa, Obeid Lutale.

Baadaye walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi mjini Kampala, ambapo walishtakiwa kwa kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria, mashtaka ambayo wanapinga.

Katika uamuzi wa kihistoria mwezi uliopita, Mahakama ya Juu ya Uganda ilitangaza kuwa ni kinyume cha katiba kwa mahakama za kijeshi kuwahukumu raia, na kuamuru kesi zote kuhamishiwa kwenye mahakama za kiraia.

Uamuzi huu ulimkasirisha Rais Museveni, ambaye alipuuzilia mbali na kuutaja kuwa “uamuzi usio sahihi,” akiapia kupinga. SOMA: Besigye afikishwa mahakama ya jeshi

Siku ya Ijumaa wiki iliyopita, Besigye, ambaye pia aligombea urais mara nne nchini Uganda, alifika mahakamani akiwa na hali ya kudhoofika kiafya.

Raia wengi wa Uganda, wakiwemo wapinzani kama Bobi Wine, walitumia mitandao ya kijamii kumtaka Besigye aachiliwe huru na aruhusiwe kupata huduma za matibabu.

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *