Mwinyi : Unganisheni Sauti ya Pamoja

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezitaka nchi wanachama wa Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) kuunganisha sauti na misimamo ili kuongeza ushawishi katika maamuzi ya kimataifa na kutetea maslahi ya nchi zinazoendelea.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo, Septemba 1, 2026, jijini Belgrade, Serbia, alipowasilisha hotuba kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa kuadhimisha miaka 65 tangu kuanzishwa kwa NAM.

Amesema misingi ya NAM bado ina umuhimu katika dunia ya sasa, akisisitiza kuwa kutofungamana na upande wowote hakumaanishi kutokuwa na msimamo, bali ni uhuru wa mataifa kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi yao na kulinda mamlaka yao.

Dk.Mwinyi ametoa wito wa kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo na upatanishi, pamoja na kufanya mageuzi katika mfumo wa Umoja wa Mataifa, hususan Baraza la Usalama, ili kuongeza uwakilishi na usawa kwa nchi zinazoendelea.

Amesema Afrika inastahili uwakilishi wa haki zaidi katika maamuzi ya kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha Ushirikiano wa Kusini na ushirikiano kati ya NAM na BRICS katika kukuza maendeleo na mageuzi ya mfumo wa utawala wa kimataifa.

Mkutano huo wenye kaulimbiu “Urithi wa Kutofungamana na Upande Wowote: Mafunzo kwa Dunia ya Leo” umehudhuriwa na viongozi na wakuu wa ujumbe kutoka mataifa 34. SOMA: Mwinyi azindua mabasi ya umeme

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button