ZLS yampa pole Rais Samia

ZANZIBAR: CHAMA cha Mawakili Zanzibar (ZLS), kimetoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, kufuatia kifo cha mume wake, Marehemu Maalim Hafidh Ameir Hassan.
Salamu hizo zimewasilishwa leo, Septemba 12, 2026, katika makazi binafsi ya Rais Dk Samia yaliyopo Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Ujumbe wa ZLS uliongozwa na Rais Mteule wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) kupitia Zanzibar Law Society, Masoud Mohamed, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Zanzibar Law Society, Shabani Mwangoda.
Katika ujumbe huo pia walikuwepo Mjumbe wa Baraza la Uongozi la ZLS, Zena Mohamed, na Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake, Vijana na Makundi Maalum, Salma Zeyn.
Kwa niaba ya uongozi na wanachama wa Zanzibar Law Society, ujumbe huo ulitoa pole kwa Dk Samia na familia yake, pamoja na ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo.

Marehemu Maalim Hafidh Ameir Hassan alifariki dunia Septemba 7, 2026, huko Zanzibar.
Zanzibar Law Society imesema inaungana na Watanzania na watu wengine walioguswa na msiba huo katika kumuombea Marehemu Hafidh Ameir Hassan.
Chama hicho pia kimewaombea wafiwa subira, faraja na nguvu katika kipindi hiki cha majonzi.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema Peponi na awape wafiwa subira na faraja. Aamiin.



