Vijana Kigoma wasifu mikopo ya halmashauri

KIGOMA: Vijana mkoani Kigoma wamesema mikopo inayotolewa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri imeleta mapinduzi makubwa katika shughuli zao za kiuchumi na maendeleo, huku ikiwasaidia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Madereva wa Bodaboda Makere, George Kagoma, amesema hayo wakati akitoa taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wazo Mwang’onda, aliyetembelea kikundi hicho.

Kagoma amesema tangu mwaka 2018 hadi sasa, kikundi hicho kimekopeshwa jumla ya Sh milioni 70.5, ambazo zimewawezesha kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Amesema baada ya kutumia mikopo hiyo katika shughuli zao, tayari wamefanikiwa kurejesha Sh milioni 50.5, huku wakipanga kuomba mkopo mwingine kwa ajili ya kununua basi la abiria litakalosaidia kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Kagoma, mikopo hiyo imewasaidia wanakikundi kuboresha maisha yao, ikiwemo kujenga nyumba, kusomesha watoto na kuhudumia familia zao.

Akizungumza baada ya kutembelea shughuli za kikundi hicho, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wazo Mwang’onda, amewataka vijana kuendelea kulinda amani na usalama wa nchi ili fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi ziendelee kuleta tija.

Mwang’onda amesema iwapo amani na usalama vitavurugika nchini, vijana hawatanufaika na mabilioni ya fedha yanayotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi, badala yake wanaweza kulazimika kukimbilia nchi nyingine kutafuta hifadhi.

Amesema Serikali imetenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya kuinua shughuli za kiuchumi za vijana, huku halmashauri zikihimizwa kutumia mapato ya ndani kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Ameongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu pekee, kwa mwaka uliopita, imetoa zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya mpango huo.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Cash earning job to earns more than $700 per day. getting paid weekly more than $3500 or more simply doing easy work online. no special skills required for this job and regular earning from this are just awesome. all you need is 2 hrs a day for this job and earning are awesome. every person can get this by follow details here…

    THIS→→→→ http://Www.Payathome1.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button