Wanawake kunufaika ushirikiano mpya

DAR ES SALAAM: WANAWAKE wajasiriamali watapata fursa ya kukuza biashara zao kwa kupata maarifa, mitaji na fursa za kujifunza katika masoko ya kimataifa.
Aidha, watapata nafasi ya kutembelea China na Uturuki ili kujifunza mbinu bora za uzalishaji, ufungashaji wa bidhaa, teknolojia na uendeshaji wa biashara zinazoweza kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.
Hatua hiyo ni baada ya Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Clouds Media Group kuingia ushirikiano mpya kupitia programu ya Malkia wa Nguvu.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam wakati wakiingia ushirikiano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Matawi na Biashara wa Benki ya CRDB, Musa Lwila, amesema benki hiyo inaamini kuwa hakuna uchumi imara unaoweza kujengwa bila ushiriki mkubwa wa wanawake katika uzalishaji, biashara na uwekezaji.

Amesema kuwa wanawake wanamiliki zaidi ya asilimia 30 ya biashara za ujasiriamali nchini, hivyo ni muhimu kuwapatia mtaji, elimu, masoko na mazingira rafiki yatakayowawezesha kukuza biashara zao na kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa.
Lwila amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Benki ya CRDB imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 700 kwa wanawake kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji. Aidha, kupitia CRDB Malkia, wanawake wameendelea kunufaika na akaunti maalumu za biashara na uwekezaji, mikopo nafuu, huduma za bima, huduma za kidijitali pamoja na mafunzo ya ujasiriamali.

Amebainisha kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka jana, zaidi ya wanawake wajasiriamali 1,000 walikuwa wamenufaika na safari za kujifunza katika nchi mbalimbali ikiwemo China na Uturuki.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Malkia Wa Nguvu Liliane Masuka na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Clouds Media Sheba Kussaga wamesema kupitia programu hiyo itawasaidia wanawake kupata Masoko ya nje na ndani na itawajengea uwezo kibiashara na itasaidia wanawake 100.



