Uhifadhi wa historia kuendelezwa Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Oman katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa kihistoria na utamaduni.

Rais Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Agosti 5, 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Katibu Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman Jamal bin Hassan Al-Moosawi, katika mazungumzo maalum yaliyohusu ushirikiano wa pande hizo mbili.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi ameipongeza Serikali ya Oman kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kupitia programu na miradi mbalimbali ya kuhifadhi urithi wa kihistoria na utamaduni. Amesema ushirikiano huo unachangia kulinda historia ya Zanzibar, kuendeleza utamaduni wake na kuongeza mchango wa maeneo ya urithi katika uchumi na maendeleo ya taifa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameihakikishia Oman ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa programu na miradi ya uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa maeneo ya urithi wa kihistoria na utamaduni. SOMA: Dkt Mwinyi akutana ujumbe Oman Zanzibar

Pia ameiomba Oman kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kupitia mafunzo na matumizi ya mbinu pamoja na teknolojia za kisasa za uhifadhi wa maeneo ya kihistoria, usimamizi wa urithi na utunzaji wa kumbukumbu. Amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha mifumo ya uhifadhi wa urithi wa Zanzibar kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman, Jamal bin Hassan Al-Moosawi, amesema Oman itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa kihistoria, utamaduni na kumbukumbu muhimu za kihistoria, kiutamaduni na kijamii.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button