Trending

Teknolojia kupunguza upotevu wa maji

(DAWASA) imeanza kutumia teknolojia za kisasa katika kufuatilia mtiririko wa maji ili kupunguza upotevu wa maji na kuimarisha huduma

DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza kutumia teknolojia za kisasa katika kufuatilia mtiririko wa maji ili kupunguza upotevu wa maji na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa mamlaka hiyo kupunguza utegemezi wa taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu changamoto za huduma, huku ikiweka mifumo itakayowezesha kupata taarifa kwa wakati na kuchukua hatua kwa haraka.

Akizungumza na HabariLeo, Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu wa DAWASA, Christian Christopher amesema uwezo wa taasisi hiyo kuitikia taarifa za changamoto umeboreshwa kwa zaidi ya asilimia 50, lakini lengo ni kufikia hatua ambayo changamoto nyingi zitatambuliwa na mamlaka yenyewe kabla ya wananchi kutoa taarifa.

Amesema kwa sasa DAWASA imeanza kutenganisha mifumo ya maji katika maeneo mbalimbali kwa kutumia flow meters, hatua inayowezesha kujua kiwango cha maji kinachoingia na kutoka katika eneo husika.

“Kwa mfano mita inaweza kuonyesha kiasi cha maji kilichoingia katika eneo fulani na kiasi kilichotoka, hivyo tofauti kati ya viwango hivyo kusaidia kubaini uwezekano wa kuwepo kwa upotevu wa maji.

SOMA ZAIDI >>https://habarileo.co.tz/aweso-akabidhi-vitendea-kazi-dawasa/

“Tunajua kutoka eneo fulani tumeingiza maji kiasi gani na tumebakiza kiasi gani. Kwa mfano, kama maji yaliyoingia ni milioni moja na yanayotoka ni laki mbili, tunajua kuna tofauti ya laki nane ambayo tunapaswa kuifuatilia,” amesema.

Amesema mfumo huo unaiwezesha DAWASA kutambua maeneo yenye upotevu mkubwa na kuelekeza rasilimali katika maeneo hayo badala ya kutegemea taarifa za wananchi pekee.

Aidha, amesema matumizi ya teknolojia yameongezwa kupitia mifumo kama SCADA, inayowezesha wataalamu kufuatilia mita na mwenendo wa mfumo wa maji kupitia vituo vya udhibiti.

Amesema hatua hiyo inasaidia menejimenti kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa sahihi na kujua maeneo yanayohitaji uwekezaji zaidi katika kupunguza upotevu wa maji.

SOMA ZAIDI

DAWASA yaanza kusafisha visima Dar

“Teknolojia ndiyo kubwa. Tunataka taarifa zetu zije kwa wakati bila kusubiri kuambiwa na wananchi, lakini pia tunataka kujua maji yanapotelea wapi ili tuweze kuchukua hatua,” amesema.

Amesema pamoja na kutumia teknolojia, DAWASA imeanza pia kuwekeza katika matengenezo kinga (preventive maintenance) ili kupunguza hitilafu na mabomba kuharibika, ambazo zinaweza kusababisha upotevu wa maji.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mamlaka hiyo pia inaangalia maeneo yenye changamoto kubwa na kuweka rasilimali za kutosha ili iweze kuitikia kwa haraka pindi taarifa zinapopatikana.

Katika hatua nyingine, alisema DAWASA inahitaji uwekezaji mkubwa katika kuongeza uzalishaji na usambazaji wa maji, hivyo ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha mipango hiyo.

Amesema mipango ya kuongeza uzalishaji na upanuzi wa huduma inahitaji fedha nyingi, ikiwemo uwekezaji katika miradi ya Kimbiji pamoja na vyanzo vingine vya maji.

Amesema mamlaka hiyo imeanza kuandaa maandiko yatakayowezesha kupata wawekezaji na washirika binafsi ili kupunguza mzigo wa uwekezaji unaobebwa na Serikali.

“Tunatafuta wadau ili jambo hili liweze kwenda haraka. Kutegemea Serikali pekee kutahitaji uwekezaji mkubwa sana, ndiyo maana tunaingiza wadau ili tuweze kwenda kwa kasi,” amesema.

Amesema pia kuna fursa ya kutumia teknolojia ya desalination katika kuzalisha maji kutoka baharini, ambayo inaweza kuwa sehemu ya suluhisho la kuongeza vyanzo vya maji katika siku zijazo.

Aidha, amesema mpango wa Serikali wa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji unalenga kuwezesha miradi mikubwa ya maji kutekelezwa kwa kasi, huku Serikali ikielekeza rasilimali zake katika maeneo mengine muhimu kwa wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button