TRA: Mfumo wa stempu umeimarisha ukusanyaji kodi

MFUMO wa Stempu wa Kielektroniki (ETS) ulioanzishwa miaka mitatu iliyopita umeimarisha ulipaji wa kodi na hivyo kuimarisha ushindani wa haki sokoni.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja Miradi wa TRA wa Mfumo wa ETS, Innocent Minja wakati akizungumzia mafanikio ya mfumo huo hapa nchini.

Alisema mfumo mpya wa ukusanyaji kodi wa ETS ulianzishwa kwa lengo la kulinda mapato ya serikali.

“Tulikuwa na changamoto kubwa ya ukusanyaji wa kodi kutokana na watu kutokuwa wa kweli na pia uwapo wa uzito katika ulipaji kodi kwa hiari.

“Awali tulilazimika kuweka maofisa wetu kuangalia uzalishaji na kuhakikisha watengenezaji wanatangaza viwango vya kweli vya uzalishaji. Hata hivyo, hali hiyo ilikuwa na changamoto nyingi na kuonekana kama vurugu tukahitaji suluhu mpya,” alisema Minja.

Aidha, alisema ufungaji wa ETS umehakikisha kuwa TRA inapata data za uzalishaji kwa wakati (muda halisi) kutoka kwa watengenezaji.

“Hii ni kwa sababu ya kodi ya ushuru kwa bidhaa maalumu hutozwa kwa kiwango cha uzalishaji hivyo kujua takwimu za uzalishaji ni muhimu.”

Akifafanua zaidi kuhusu ujio wa mfumo huo uliofungwa mara mbili alisema kutokana na wakusanya kodi kukabiliwa na changamoto ya kujua viwango vya kweli vya kodi kwa uzalishaji uliopo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifikiria kutafuta njia nyingine ya kisasa na sahihi ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Kazi ya kupata mfumo sahihi kukabiliana na changamoto hiyo ilipewa kampuni ya Uswisi, ya Societe Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (SICPA). Kampuni hii ilikuja na mfumo wa stempu wa kielektroniki (ETS).

Alisema katika kufanikisha utendaji wake, TRA iliweka awamu kadhaa za utekelezaji wa mfumo, ambapo katika awamu ya kwanza ya mfumo, iliyozinduliwa Januari 15, 2019 stempu za kielektroniki ziliwekwa kwa kampuni 19 zinazozalisha bidhaa za pombe, mvinyo na vinywaji vikali nchini.

Awamu ya pili ya stempu za kielektroniki iliyoanza Agosti 1, 2019 ziliwekwa kwenye bidhaa kama vile maji yaliyotiwa ladha tofauti na kwenye vinywaji vingine visivyo vya kileo.

“Mfumo ulileta uwazi kwenye kodi hasa kwenye kodi ya ushuru, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi ya kampuni na hatimaye kupunguza manung’uniko ya walipa kodi,” alisema Minja.

Alisema mchakato wa ufungaji ni endelevu haswa kutokana na viwanda kuendelea kuongeza uwezo na mifumo ya mitambo ikiwamo kujiendesha yenyewe.

“Tayari tumeweka mfumo wa ETS kwa watengenezaji wote wanaostahiki wa bidhaa maalumu. Takribani vifaa 135 vimefungwa kwenye viwanda vyenye mitambo inayojiendesha huku viwanda visivyojiendesha vikilazimika kuwasha mfumo huo kila wanapoanza uzalishaji,” anasema Minja.

Pamoja na kufanikisha ukusanyaji wa mapato mfumo huo pia umewezesha wazalishaji wa bidhaa kujua kiasi cha bidhaa zinazoingizwa sokoni kutoka nje, hivyo kusaidia kuwapatia taarifa wazalishaji wa ndani nini wakifanye ili kuhami bidhaa zao sokoni dhidi ya zile zinazotoka nje.

Minja aliongeza kwamba, ETS sio tu imerahisisha kadirio la makusanyo ya kodi, lakini pia mfumo umesaidia wazalishaji kutambua kiasi cha uzalishaji na muda ulitumika kuzalisha bidhaa husika. Pia imesaidia kujua changamoto zinazohusiana na mchakato wa uzalishaji na kutafuta suluhu za changamoto hizo.

Pia mfumo wa ETS ukitumika vyema utarahisisha ulipaji na ukusanyaji wa mapato kwa wafanyabiashara.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button