‘Tafiti zitumike kutatua changamoto kwa jamii’

JAMII inapaswa kunufaika na majibu chanya ya kisayansi yanayopatikana kupitia tafiti zinazofanywa kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali ulimwenguni.

Ofisa Mkuu Uendeshaji kutoka Taasisi ya Sayansi Afrika (SFA), Ragnold Zondo, ameeleza hayo wakati wa uzinduzi wa tuzo za uandishi wa habari za sayansi Afrika uliofanyika nchini Zambia.

Amesema ili jamii inufaike na taarifa hizo za kitafiti, SFA inawezesha wanahabari kuandika habari za kisayansi ambazo zinatoa majibu ya changamoto mbalimbali katika jamii.

Amekiri kuwa Afrika kuna changamoto katika kuandika habari za kisayansi lakini inapaswa kuzibadili ili ziwe fursa kwa jamii.

Amesema taasisi hiyo imeamua kuanzisha tuzo za uandishi wa habari za sayansi ili iwe kichocheo kwa waandishi wa habari wachanga kupenda kuziandika.

“Waandishi wanapaswa kueleza kuwa sayansi inabadili changamoto ulimwenguni kwa kuwa kupitia sayansi maisha yataboreshwa,” amesema.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa Biashara na Sayansi SFA, Deborah-Fay Ndlovu, amesema taasisi hiyo inatoa tuzo kutambua mchango wa wanahabari wanaoripoti habari za sayansi.

“Ahadi yetu ya kuongeza uwezo wa wanahabari wa Kiafrika kuripoti habari za sayansi inatokana na imani kwamba jamii yenye ufahamu wa kutosha ni chachu ya maendeleo.

“Kuwawezesha wanahabari kuzama ndani ya mambo magumu ya sayansi sio tu kunakuza uandishi sahihi bali pia kunakuza utamaduni wa uchunguzi na uvumbuzi, muhimu kwa maendeleo endelevu ya bara letu.

“Kwa kuwekeza katika ujuzi na maarifa ya wanahabari wa Kiafrika, tunatayarisha njia kwa siku zijazo ambapo mawasiliano ya kisayansi yanakuwa msingi katika kuunda sera, kukuza uelewa wa umma, na hatimaye kuboresha maisha ya jamii zetu,” amesema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button