Viongozi wa umma wafundwa maadili

MOROGORO: OFISI ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imesema katika mazingira ya sasa ya utumishi wa umma mafunzo ya maadili kwa viongozi ni suala muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho kuna mtanziko mkubwa wa changamoto za kimaadili kuanzia ngazi ya familia , taasisi za umma na jamii kwa ujumla.

Kamishna wa Maadili Sekretarieti hiyo, Jaji Mstaafu ,Silvangilwa Mwangesi amesema hayomjini Morogoro katika ufunguzi wa mafunzo ya maadili ya viongozi wa umma ambao ni Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Taasisi na Mashirika ya umma , makatibu tawala wasaidizi wa mikoa (ASS) na Makatibu Tawala wa wilaya
Hotuba ya ufunguzi ilisomwa kwa niaba yake na Katibu Mtendaji Mstaafu, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma , Mathew Kirama ambaye pia ni kiongozi wa timu ya wawezeshaji wa mafunzo hayo.

Jaji Mstaafu Mwangesi amesema kuwa uongozi wenye maadili huimarisha imani ya wananchi kwa serikali na taasisi zake .
Amesema wananchi wanapowaona viongozi wao wakitenda kwa haki, uwazi na uadilifu, huongeza ushirikiano, utii wa sheria na mshikamano katika jamii iliyowazunguka.
Jaji Mstaafu Mwangesi amesema maadili ni kinga ya maovu yote na nguzo muhimu ya utawala bora na maendeleo endelevu wa taifa.

Amewataka wakawe mabalozi wa mabadiliko katika utumishi wa umma na baada ya mafunzo hayo Ofisi ya Rais inatarajia kuona matokeo chanya kwenye taasisi zao zitakazotokana na matunda ya mafunzo hayo na kwamba Ofisi ya Maadili itafuatilia.
Naye, Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka Kanda ya Kaskazini, Gerald Mwaitebele amesema mafunzo hayo ya siku tatu yalianza Aprili 15 na kufikia tamati Aprili 17, 2026.
Amesema mada mbalimbali zitafundishwa ambazo ni pamoja na changamoto za uongozi kimaadili, utawala bora, viongozi katika utumishi wa umma na shinikizo la kuoanisha misingi ya utawala bora.
Mwaitebele ambaye ni mratibu wa mafunzo hayo ametaja baadhi ya nyingine ni matakwa ya kisiasa, matarajio ya umma, migongano ya maslahi na matamko ya viongozi wa umma na changamoto za mapambano dhidi ya rushwa katika taasisi za umma .
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama , mkoani Shinyanga ,Glory Absalum kwa niaba ya washiriki wenzake amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo na kukumbushwa majukumu mbalimbali ambayo wao wakiwa ni viongozi wanatakiwa kuyasimamia kikamilifu.
“Siku tatu hizi tumejifunza mambo mengi na kupata nyenzo mpya za kwenda kusimamia utekelezaji wa majukumu yetu na kuongeza utoaji wa huduma kwa wananchi ambazo wanazipata kila siku,” amesema Glory.



