Wafungaji bora wa muda wote AFCON

MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 (AFCON) inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 13 nchini Ivory Coast.

Mataifa 24 yamefuzu, michuano hiyo ya 34 inabaki kuwa michuano mikubwa kwa ngazi ya mataifa Afrika, ikionyesha vipaji vya juu na ushindani wa uliotukuka.

Kihistoria, majina kama Samuel Eto’o na Didier Drogba yanaongoza kwa kufanya makubwa katika michuano hiyo, hasa kwa umahiri wao wa kupachika mabao.

Tamaduni hii inaendelea katika mashindano ya sasa, huku wachezaji kama Mnigeria Victor Osimgen na Mcameroon Vincent Aboubakar wakilenga kufikia mafanikio ya watangulizi hao.

Wakati AFCON ya 2023 ikikaribia, HabariLeo imekusogezea wafungaji bora zaidi wa mashindano hayo. Wachezaji kama Andre Ayew (Ghana), mwenye mabao 10, na Aboubakar (Cameroon), mwenye mabao 9, wanakaribia kufikia rekodi za wachezaji hao.

SAMUEL ETO’O – MABAO 18

Mchezaji Bora wa Afrika mara nne Samuel Eto’o anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya mashindano hayo, baada ya kuzifumania nyavu mara 18.

Baada ya kuitumikia Cameroon mwaka wa 1996 akiwa na umri mdogo tu wa miaka 16, Etoo akiwa na timu hiyo alishinda AFCON mwaka wa 2000 na 2002. Aliibuka mfungaji bora mara mbili mwaka 2006 na 2008, alipofunga mabao matano

LAURENT POKOU – MABAO 14

Kabla ya Didier Drogba, Ivory Coast walikuwa na mshambuliaji mwingine maarufu Laurent Pokou. Mchezaji huyo alifunga mabao 14 katika michezo 13 pekee ya AFCON, wastani wa mabao 1.17 kwa kila mchezo.
Pokou alifunga bao lake la AFCON katika mwaka 1968, akihitimisha kampeni yake ya kwanza kwa mabao sita katika mechi tano.
Mwaka uliofuata 1970, mshambuliaji huyo alifunga mabao manane katika michezo mitano, likiwemo la ushindi wa mabao matano dhidi ya Ethiopia, rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa.

RASHID YEKINI – MABAO 13

Wakati Nigeria ikielekea AFCON 2023 huku Victor Osimhen akitazamiwa kuwa ndiye mchezaji hatari zaidi timu hiyo, usisahau kwamba Super Eagles walikuwa na mmaliziaji hatari Rashid Yekini.

Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Nigeria mwenye kumbukumbu nzuri anashika nafasi ya tatu kati ya wafungaji bora wa michuano hiyo, akiwa na mabao 13 katika mechi 24 katika matoleo manne.

Alikuwa mfungaji bora katika mwaka 1992 akiwa na mabao manne, na mwaka 1994 alipofunga mabao matano.

HASSAN EL-SHAZLY – MABAO 12

Licha ya uwepo wa wachezaji hatari kwenye kikosi cha Misri kama vile Mohamed Salah na wengine waliowahi kucheza kama Ahmed Mido aliyewahi kupita klabu kadhaa EPL ikiwemo Wigan, Tottenham na Middlesbrough, lakini Hassan El-Shazlyb alikuwa hatari.

El-Shazly alionekana kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo mwaka 1963. Alifunga mabao sita na kuishia kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo, na kuiongoza Misri kumaliza katika nafasi ya tatu. Mnamo 1970, alifunga mabao matano wakati Misri ikimaliza nafasi ya tatu.

PATRICK MBOMA – MABAO 11

Mmoja wa wanasoka mahiri wa Cameroon, Patrick Mboma alijihakikishia nafasi kati ya ufungaji bora wa michunao ya Afrika katika mashindano ya kwanza.

Mnamo mwaka 2000, Mboma sio tu alishinda Kombe la Mataifa ya Afrika lakini pia alijishindia medali ya dhahabu ya Olimpiki akiwa na ‘Indomitable Lions’.

HOSSAM HASSAN – MABAO 11

Hossam Hassan aliiwakilisha Misri kwenye michuano saba tofauti ya AFCON huku akijipatia mabao 11 katika mechi 21.

Akiwa na umri wa miaka 40, Hassan aliwahi kuwa nahodha wa Mafarao wa Misri wakati wa Kombe la Mataifa ya Afrika la 2006. Huu ulikuwa ushindi wake wa tatu wa bara na hitimisho la kuonekana kwake katika mashindano haya.

DIDIER DROGBA – MABAO 11

Drogba alicheza mechi yake ya kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2006, akihitimisha michuano hiyo kwa mabao matatu, ingawa Cote d’Ivoire ilishindwa katika fainali na Misri kwa mikwaju ya penalti.
Mshambulizi huyo aliongeza mabao matatu mwaka 2008, huku Ivory Coast ikishika nafasi ya nne.

Ushiriki wake ulikuwa mdogo katika AFCON 2010, iliyoshirikishwa katika mechi tatu pekee na kufunga bao moja.

Mnamo 2012, Drogba alifunga mara tatu Ivory Coast ikimaliza washindi wa pili. Mechi yake ya mwisho ya AFCON mwaka 2013 ilimfanya kufunga bao moja pekee.

Wachezaji wengine Ndaye Mulamba wa DR Congo, Francileudo Santos wa Tunisia, Joel Tiéhi wa Ivory Coast, Mengistu Worku raia wa Ethiopia, Kalusha Bwalya wa Zambia na Andre Ayew hawa wote walihitimisha safari yao ya kuzitumikia timu zao kwenye michuano hii wakiwa na mabao 10.

Habari Zifananazo

Back to top button