Mamelodi yaacha gumzo Afrika

AFRIKA KUSINI: Timu ya Mamelodi Sundowns (Masandawana) ya Afrika Kusini imeacha gumzo kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutupwa nje ya michuano hiyo jana usiku.

Mamelodi wameondoshwa na Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya kupoteza michezo miwili ya nyumbani na ugenini.

Wababe hao wa soka la Afrika Kusini ni moja ya vilabu vyenye kikosi ghali zaidi barani Afrika na moja ya timu tishio kwasasa katika soka la ngazi ya vilabu barani humu.

Advertisement

Mbali na matarajio ya wengi wababe hao kwa mara nyingine tena wameshindwa kufuzu Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiishia hatua ya Nusu Fainali kama ilivyokuwa msimu jana.

Ukurasa ambao mashabiki wa ‘Masandawana’ hawatopenda kuusoma katika simulizi ya michuano ya msimu huu ni timu yao kushindwa kufunga bao katika michezo minne mfululizo wakianzia michezo miwili ya Robo Fainali dhidi ya Yanga na michezo miwili ya Nusu fainali dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Licha ya uwekezaji mkubwa wa timu hiyo bado kitendawili cha ubingwa wa Afrika kimekuwa kigumu kwani mara ya mwisho kutwaa Ligi ya Mabingwa ilikuwa ni Mwaka 2016, tangu hapo kitu pekee wanachojivunia kuhusu soka la Afrika ni ubingwa wa African Football League waliotwaa mwaka jana.