Kampuni yatangaza fursa za michezo kuelekea AFCON 2027

DAR ES SALAAM: WAKATI Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027, kampuni ya T9 imeibuka na mkakati wa kuhamasisha Watanzania kuzitumia fursa za kiuchumi zitakazoambatana na mashindano hayo kupitia uzinduzi wa jarida la T9 Magazine Opportunity Plus.

Akizungumza katika uzinduzi huo Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa T9, Othman Razak, amesema AFCON si mashindano ya mpira pekee bali ni jukwaa kubwa la biashara, utalii na uwekezaji ambalo linaweza kubadili maisha ya Watanzania wengi.

“AFCON ni mwanzo wa fursa kubwa. Tunataka Watanzania wajue namna ya kunufaika na ujio wa wageni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na duniani,” amesema Razak huku akihimiza wadau, makampuni na Taasisi mbalimbali kutangaza nao ili kutumia nafasi ya kutangaza fursa.

Amesema jarida hilo limeandaliwa maalumu kuonesha maeneo mbalimbali yatakayoweza kunufaika na mashindano hayo ikiwemo sekta za hoteli, usafiri, chakula, biashara ndogondogo na utalii.

“Leo ni siku kubwa ya furaha kwetu. Tunazindua jarida lenye manufaa makubwa ambalo linagusa uchumi, afya na michezo. Tumefuata mfano mzuri wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuleta maendeleo yenye kugusa watu,” amesema Razak.

Amesema kupitia AFCON, Watanzania wanapaswa kuanza kujiandaa kunufaika kiuchumi na kwamba T9 itakuwa sehemu ya kuwaunganisha wafanyabiashara na wadau mbalimbali ili kuona namna bora ya kutumia fursa hizo.

Aidha amesema jarida hilo pamoja na tovuti ya T9 vitakuwa vikitoa taarifa mbalimbali kuhusu maendeleo ya michezo, biashara na uwekezaji huku akibainisha kuwa toleo jingine la jarida hilo linatarajiwa kutoka mwezi ujao.

Kwa upande wake, mwandishi wa michezo wa Clouds Media, David Kampista, amesema jarida hilo litasaidia kufungua fikra za watu kuhusu fursa zilizopo kupitia michezo na AFCON.

“Jarida hili linakwenda kutufungua zaidi kuona fursa zilizopo. Ni vizuri kila mmoja akaruhusu mawazo mapya kwa sababu michezo sasa ni sehemu ya uchumi,” amesema.

Naye mwandishi mwandamizi wa michezo wa TBC, Malyo Njedengwa maarufu ‘Super Coach’, amesema uwekezaji mkubwa uliofanyika katika bandari umeifanya Tanzania kuwa lango muhimu la biashara Afrika Mashariki na Kati, jambo litakaloongeza idadi ya wafanyabiashara na wageni watakaokuja nchini wakati wa AFCON.

“Ukizungumzia AFCON unazungumzia fursa kubwa sana. Hoteli zitafanya vizuri, usafiri utaongezeka, hata biashara ndogo ndogo kama vyakula, kahawa na huduma za usafiri zitapata wateja wengi kabla na baada ya mechi,” amesema.

Malyo amesema kupitia jarida hilo, wageni watakaokuja Tanzania wataweza kupata taarifa muhimu za maeneo ya kutembelea, hoteli na huduma mbalimbali zinazopatikana nchini, hatua itakayosaidia kukuza utalii na uchumi kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button