Ayoub atoa Sh milioni 21 kuimarisha michezo Unguja

ZANZIBAR: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, ametoa mchango wa Sh milioni 21 kwa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ajili ya kusaidia utoaji wa zawadi na uendeshaji wa shughuli za michezo.

Lengo ni kuondoa changamoto ya ukosefu wa zawadi iliyokuwa ikiathiri mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu kwa takribani miaka mitatu mkoani humo.

Mchango huo ameukabidhi kwa viongozi wa michezo mkoani humo wakati wa kuhitimisha mchezo wa fainali wa soka uliowakutanisha timu ya Kitope na Mundu, ambapo timu ya Kitope iliibuka na ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Mundu katika mchezo uliovutia mashabiki wengi.

Aidha, Naibu Waziri amesema fedha hizo zitatumika kufanikisha utoaji wa zawadi kwa timu zilizoshiriki mashindano ya misimu iliyopita pamoja na msimu wa sasa, hatua inayolenga kurejesha hamasa ya michezo kwa vijana na kuimarisha maendeleo ya soka katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kadhalika, Ayoub amebainisha kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa michezo katika kujenga afya, kukuza uchumi na kuimarisha mshikamano wa jamii, huku akisisitiza umuhimu wa vijana kutumia michezo kama nyenzo ya kujiletea maendeleo badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuharibu maisha yao.

Katika hatua nyingine, Ayoub amewaasa vijana kuachana na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na badala yake kutumia michezo kama njia ya kujenga afya, uchumi na mshikamano wa jamii ili kujiletea maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Vilevile, amewahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuhakikisha usalama katika maeneo yote yanayofanyika shughuli za michezo ili wananchi waweze kushiriki michezo kwa amani na utulivu, huku akiwataka wachezaji kucheza wakizingatia nidhamu

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button