‘Udhamini NBC umechangia ushindani Championship’

DAR ES SALAAM; MDHAMINI Mkuu wa Ligi Daraja la Kwanza (NBC Championship), Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi kombe la ubingwa wa ligi hiyo kwa timu ya Kengold yenye maskani yake Wilayani Chunya, mkoani Mbeya ambayo ndiyo bingwa wa ligi hiyo msimu wa 2023/2024.

Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika  jana Uwanja wa Azam Complex  jijini Dar es Salaam, ikipambwa na mechi ya kirafiki kati ya bingwa huyo na timu ya Pamba FC mechi iliyoisha kwa timu hizo kufungana bao 1-1. Pamba na Kengold zote zitacheza Ligi Kuu msimu ujao.

Mkurugenzi wa Biashara wa benki ya NBC, Elvis Ndunguru alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi kwenye tukio hilo lililopambwa na uwepo wa Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mbaraka Batunga likihushuhudiwa pia na mamia ya wapenda soka wakiwemo mashabiki waliosafiri kutoka mikoa ya Mbeya na Mwanza. Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Steven Mnguto alimuwakilisha Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Akizungumza kwenye makabidhiano hayo, DC Batunga alisema pamoja na kuipongeza Kengold kwa kuibuka kinara wa ligi hiyo, ameishukuru benki ya NBC kuwa mdhamini wa ligi hiyo.

Amesema udhamini huo kwa kiasi kikubwa umechochea ushindani kwenye ligi hiyo, hatua ambayo anaamini imesaidia kutoa washindi wenye sifa ya kushiriki Ligi Kuu kwa sifa na vigezo vinavyotakiwa na wapenda soka.

“Udhamini wa NBC umewezesha kuongeza ushindani kwenye ligi hii na kuboresha soka letu. Leo hii sisi Wanachunya tunajivunia kuwa washindi wa ligi iliyokuwa na ubora kama tulioushuhudia na kupitia ushindani huo tunaamini tunakwenda kutoa changamoto haswa kwenye timu tutakazokutana nazo ligi kuu ya NBC. 

“Baada ya ubingwa huu tunakwenda kujipanga kuanzia kikosi hadi benchi la ufundi ili kujiweka sawa zaidi kwa ajili ya Ligi Kuu ya NBC…tunawakaribisha sana Chunya,’’ amesema.

Kwa upande wake Ndunguru amesema benki hiyo inayodhamini ligi tatu muhimu hapa nchini, itaendelea kuboresha zaidi ligi hizo ili ziendelee kutoa matokeo chanya kulingana na malengo ya udhamini huo ikiwemo suala zima la kuzalisha ajira ambapo kwa sasa jumla ya ajira 7,000 za moja kwa moja zimezalishwa kupitia udhamini huo.

“Tunawapongeza sana washiriki wote wa ligi ya Championship, lakini kiupekee zaidi tunawapongeza Kengold kwa kuibuka washindi kwenye ligi hii.

“Pongezi zetu pia tunazielekeza Pamba FC kwa kuwa mshindi wa pili na hivyo nae pia anakwenda kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao…hongereni sana,’’ alisema Ndunguru.

 

Akizungumzia ubingwa huo, nahodha wa Kengold Charles Masai pamoja na kuwashukuru wadau wote kwa jitihada zao zilizosaidia kufanikisha ubingwa huo akiwemo mdhamini huyo kwa kuandaa mazingira mazuri kwa timu zote shiriki, aliahidi kwa niaba ya wachezaji wenzake kuhakikisha wanajipanga vyema ili waweze kutoa ushindani zaidi kwenye ligi msimu ujao

 

Habari Zifananazo

Back to top button