‘Bureau de change’ zilizofungwa sasa kufunguliwa

DODOMA: Serikali ipo mbioni kufungulia maduka ya kubadilisha fedha nchini (Bureau de change), ambayo yalifungiwa mwaka 2016 kutokana na tuhuma za utakatishaji fedha, huku wabunge wakitaka maduka yasiyo na hatia yalipwe fidia.

Akizungumza leo Aprili 2, 2024 Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan haipo tayari kuona rasilimali na fedha za mtu yeyote zilizochukuliwa zimebaki serikalini.

Chande alikua akijibu swali la Mbunge wa Chumbuni, Ussi Salum Pondeza aliyehoji  sababu zilizosababisha maduka ya kubadilisha fedha kuondolewa katika biashara na wananchi wengi kupoteza ajira zao.

Chande amesema serikali itayafungulia maduka hayo muda wowote kuanzia sasa na kurudishiwa mali na fedha zao zote zilizopokwa na serikali katika operesheni iliyofanyika mwaka 2019.

“Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge (Ussi Salum Pondeza) wale wote ambao maduka yao hayana makosa watarejeshewa fedha zao na mali zao, lakini nimpe taarifa tu mwaka ule maduka  68 ndio yalifungwa, tayari tumeshafungulia maduka 61  yaliyobaki ni saba na yatafunguliwa muda wowote,” amesema.

Anasema serikali ilichukua uwamuzi wa kufungia maduka hayo ya kubadilisha fedha mwaka 2016, baada ya Benki Kuu ya Tanzania  kufanya ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na kugundua miamala mbalimbali kwa baadhi ya maduka, kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za usimamizi wa maduka ya fedha za kigeni.

Pia BoT ilifanya udhibiti  wa utakasishaji wa fedha haramu. Kufuatia hali hiyo, mwaka 2018 na 2019, BoT kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za serikali ilifanya operesheni ya ukaguzi maalum kwenye maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni nchini na kubaini makosa mbalimbali,  ikiwemo kutofanya utambuzi wa wateja kabla ya kutoa huduma kinyume na kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Udhibiti wa Utakatishaji Fedha Haramu, Sura 423 na kanuni ya 17 ya Kanuni za Udhibiti wa Utakatishaji Fedha Haramu;

“Kugawa miamala ya wateja kwa lengo la kukwepa kutunza kumbukumbu muhimu zinazoonesha uhalali wa miamala kinyume na Kanuni ya 23(4) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015 na kutokutoa stakabadhi za miamala kinyume na Kanuni ya 23(1) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015,” amesema Chande

Pia amesema maduka ya kubadilisha fedha yalikuwa hayawasilishi  taarifa sahihi za miamala benki kuu na hivyo kuathiri upatikanaji wa takwimu muhimu kwa ajili ya sughuli za kiuchumi; na baadhi ya maduka yalikuwa yanajihusisha na uhamishaji wa fedha nje ya nchi bila kuwa na leseni wala kibali cha Benki Kuu.

 

Habari Zifananazo

Back to top button