ADC wampongeza Samia kuruhusu mikutano ya siasa

CHAMA Cha Alliance For Democratic Change (ADC)  kimempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuondoa zuio la kufanyika kwa mikutano ya Vyama vya Siasa nchini ambayo kwa zaidi ya miaka miwili  ilikuwa imezuliwa.

Akizungumza Dar es Salaam Leo mara baada ya kumalizika kwa mkutano baina ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan  na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa katika Viwanja vya Ikulu Dar es Salaam,  Katibu Mkuu  wa ADC Doyo Hassan Doyo amesema hatua hiyo ya Dk Samia inaonyesha busara na hekima alizonazo katika kulingoza Taifa.

” Rais Dkt Samia !meonyesha alama kubwa hapa nchini katika uongozi wake, kitendo hiki alichokifanya siyo kitampa heshima  hapa Tanzania bali duniani kote kwa kuwa siasa ni kitu kinachotambulika kila mahali” amesema Doyo

Awali akizungumza na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa katika Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ametangaza kuondolewa kwa zuio la kufanyika kwa mikutano hiyo ya vyama vyote vya siasa kwa kusema hiyo ni haki yao kikatiba huku akivitaka kuheshimu taratibu za sheria juu ya taratibu za uendeshaji wa mikutano yao.

“Wajibu wenu ni kufuata sheria zinavyosema ni kufuata kanuni zinavyosema, lakini kama waungwana kama wastaarabu Watanzania wenye sifa ndani ya Dunia hii niwaombe sana, tunatoa ruhusa twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, siasa za kupevuka, tukafanye siasa za kujenga sio kubomoa.” amesema Dk Samia.

Pamoja na hilo Dkt Samia Rais Dk Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba kwa namna watakavyokubaliana na vyama vingine vya upinzania.

“Kuna haja ya kuangalia hali halisi ya sasa hivi, je yale yaliyomo mule mangapi yanatufaa na mangapi hayatufai, tunakwendaje, lengo ni kuona tunafika mahali pale tulipokusudia ” amesema Rais Dk Samia.

Amesema muda wowote kuanzia sasa itaundwa kamati maalumu ambayo itashauri namna ya kuendesha mchakato huo ambayo itahusisha watu wa makundi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa, vya kijamii, Watanzania walioko International Communities, Wawakilishi wa vyombo vya usalama, watakuwemo kwenye hiyo kati ili waje na kitu ambacho kitakuwa cha Watanzania.”ameongeza Rais Dk Samia.

Aidha akizungumzia hayo Doyo amesema wao kama ADC dhamira yao ni kufanya siasa za kistaarabu hivyo watafanya mikutano yao kwa lengo la kutangaza ilani na sera zao kwa wananchi ambazo kwa kipindi kirefu walikosa.

Amesema katika utekelezaji wa hilo ADC imepanga kuanza kufanya ziara ya mikoa ya kigoma Tanga,Lindi mtwara na mwanza kufanya mikutano ya hadhara itakayo ongozwa na viongozi wa kitaifa

 

Habari Zifananazo

Back to top button