ACT Wazalendo kutoa nafasi kwa wanawake
DAR ES SALAAM; NAIBU Mwenezi wa Chama cha ACT Wazalendo, Shangwe Ayo amesema chama hicho kitaendelea kuwapa nafasi wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Akizungumza na HabariLEO kuhusu nafasi ya wanawake leo Aprili 9, 2024, Shangwe amesema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kiutendaji na ndio maana chama hicho kinaendelea kuwaamini.
“Tuna wanawake wengi wenye uwezo, sasa kwa sababu chama chetu kina wanawake wengi wenye uwezo tunasema kwa nini tusiwapa nafasi wakaendelea kuonesha uwezo wao,” amesema Shangwe.
Shangwe amesema Machi 2, 2024 kwenye mkutano mkuu wa wanawake walizindua sera ya ushiriki wa wanawake kwenye masuala ya siasa, hivyo chama hicho kitaendelea kuwapa wanawake ushiriki katika masuala mbalimbali.
Amesema chama hicho kina idara tano zenye watendaji 10, ambapo wanawake ni sita na wanaume wanne.
Amesema Bodi ya Wadhamini ya chama, mwenyekiti na katibu ni wanawake na wanafanya vizuri , ambapo pia asilimia 50 ya wajumbe wa Kamati Kuu ni wanawake na asilimia 50 wajumbe wa Halmashauri Kuu ni wanawake.