Ubora wa miradi uendane na thamani ya fedha

GEITA: Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amesema miradi ya maendeleo inayotekelezwa iendane na thamani ya fedha inayotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji.
Kihongosi ametoa kauli hiyo leo Aprili 17,2026 alipokagua mradi mkubwa wa Sh bilioni 22 unaotekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa Geita mkoani Geita akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Kihongosi amesema miradi hiyo ya maendeleo wanayoiona hapo Geita, jambo la msingi ambalo wanalisisitiza sana ni ubora wa kazi dhidi ya thamani ya fedha inayotumika.
“Hatutaki miradi ya kukamilika tu kwa ajili ya kutumika, tunataka miradi ambayo kila shilingi inayotumika inaonekana kwenye matokeo yake. Hiyo ndiyo maana ya thamani ya fedha (value for money).

Ameongeza; “Mradi huu wa zaidi ya Sh bilioni 22 wa barabara na miundombinu ya stendi, ni mfano halisi wa namna serikali inavyosisitiza ubora licha ya changamoto zilizojitokeza, hatukuruhusu kazi ishuke kiwango”.
Akisisitiza kuwa hiyo ndoyo tafsiri halisi ya matumizi bora ya fedha za umma, si suala la kukamilisha mradi tu, bali ni kuhakikisha miundombinu inayojengwa inadumu, inahudumia wananchi kwa muda mrefu na inatoa thamani halisi ya fedha iliyowekezwa.

“Kwahiyo, tunapozungumza miradi ya maendeleo, tujue wazi kwamba ubora ndio msingi, na thamani ya fedha ndio dira yetu,” amesisitiza Kihongosi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Barnabas Mapande amewataka watumishi waumma na watekelezaji wa miradi kuwa wawajibikaji wa kweli na si kuvizia ugeni mkubwa wa iongozi ndo wanajifanya wanakazana kufanya kazi.
Akitoa taarifa ya utekelzaji wa mradi huo Mkurugeniz wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Yefred Muyenzi amesema ni mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC)wa Sh bilioni 22 unahusisha ujenzi wa kilomita 17 za barabara kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa Stendi ya Kisasa katika eneo la Magogo.
Amesema huo unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia awamu mbalimbali katika miji ya Tanzaniana mradi wa barabara unatekelezwa na mkandarasi Sichuan Road and Bridge Corporation kwa miezi 15.
Mradi ulianza rasmi Novemba 20, 2023 na ulitarajiwa kukamilika Februari 2025, lakini ulikumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kuchelewa kwa vifaa, mabadiliko ya bei za vifaa, hali ya hewa na mtiririko mdogo wa fedha, hivyo sasa unatarajiwa kukamilika Novemba 30,2026.



