CCM yakoshwa na mradi wa umwagiliaji Iringa

IRINGA: Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa imeeleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi miwili mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na wilayani Iringa, ikisema uwekezaji huo unachochea uchumi wa Iringa kwa kuunganisha uzalishaji wa kilimo, usafiri wa anga na fursa za uwekezaji.
Katika ziara yake ya ukaguzi, kamati hiyo ilitembelea skimu ya umwagiliaji Mkombozi iliyopo Tarafa ya Pawaga pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria na maegesho ya magari (Phase II) katika Uwanja wa Ndege wa Iringa.

Miradi hiyo kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James inatajwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa unaobeba mustakabali wa maendeleo ya mkoa wa Iringa na Nyanda za Juu Kusini.
“Taswira inayojitokeza ni kwamba Serikali haijajenga tu miundombinu, bali inaunganisha sekta zinazotegemeana; kuongeza uzalishaji mashambani huku ikipanua uwezo wa mkoa kufikia masoko, wawekezaji na watalii kupitia usafiri wa anga,” James alisema.

Mradi wa kkimu ya umwagiliaji Mkombozi wenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 56 umefikia asilimia 95 ya utekelezaji na unatarajiwa kukabidhiwa rasmi mwezi Septemba mwaka huu.
Maafisa wa mradi waliieleza Kamati ya Siasa kuwa mradi huo umeundwa kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa kilimo cha umwagiliaji, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula pamoja na kipato cha wakulima.
Mradi huo utapanua eneo la umwagiliaji kutoka ekari 4,500 zilizokuwa zikitegemea mifereji ya asili hadi ekari 15,000, huku uzalishaji wa mpunga ukitarajiwa kuongezeka kutoka wastani wa tani mbili hadi tani tano kwa hekta kutokana na matumizi ya teknolojia na mbinu bora za kilimo.

Kwa wakulima wa Pawaga, mradi huo ni mwisho wa utegemezi wa mifereji ya asili iliyokuwa ikiharibiwa mara kwa mara na mafuriko, hali iliyokuwa ikisababisha hasara kubwa kwa uzalishaji.
Mwenyekiti wa Skimu ya Umwagiliaji Mkombozi, Chesco Msamba, alisema mradi huo umeleta matumaini mapya kwa maelfu ya wakulima.

“Tulikuwa tunaanza upya kila mvua kubwa iliponyesha kwa sababu mifereji ilikuwa ikiharibika. Sasa tuna uhakika wa maji na tunaona mustakabali mpya wa kilimo chetu,” alisema.
Msindikaji wa mazao, Lukas Ndete, alisema ongezeko la uzalishaji limeongeza uwezo wa kiwanda chake kukoboa mpunga kutoka magunia 10,000 hadi kufikia magunia 27,000, hatua inayoongeza ajira na shughuli za biashara katika eneo hilo.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, alisema mradi huo utaifanya Pawaga kuwa moja ya maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mpunga nchini.
Alisema Serikali imeanza pia kutatua changamoto zinazoweza kuhatarisha uwekezaji huo kwa kutenga maeneo maalumu ya kunyweshea mifugo ili kulinda miundombinu ya umwagiliaji, sambamba na kuendelea na zoezi la upimaji wa mashamba na utoaji wa hati za ardhi ili kuimarisha kilimo cha kisasa.
Akitoa ujenzi wa jengo jipya la kisasa la abiria katika uwanja wa ndege Iringa, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Hosea Machaka, alisema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 250,000 kwa mwaka na kupokea abiria 150 kwa wakati mmoja.

Alisema mradi huo pia unahusisha ujenzi wa maegesho ya magari, barabara za ndani, mifumo ya kupitisha maji pamoja na taa na alama za usalama, huku ukitekelezwa kwa kutumia nguvu kazi ya wananchi ambapo ajira 165 tayari zimezalishwa.
Kwa mujibu wa Kamati ya Siasa, uwanja huo utakuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta za utalii, biashara, usafirishaji na uwekezaji kwa kuifanya Iringa kuwa lango muhimu la Nyanda za Juu Kusini.
Daudi Yassin alisema Kamati imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kupongeza Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi inayobadili maisha ya wananchi.
“Miundombinu hii itafungua fursa mpya za kiuchumi. Watalii, wawekezaji na wafanyabiashara watafika kwa urahisi zaidi, na wananchi watanufaika kupitia biashara na huduma mbalimbali,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, alisema uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Iringa ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Iringa kuwa kitovu cha biashara, uwekezaji na utalii katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Aliongeza kuwa matumizi ya nguvu kazi ya wazawa katika utekelezaji wa miradi hiyo yameongeza ajira na kipato kwa wananchi, huku akiwahimiza kujipanga kutumia fursa zitakazozaliwa baada ya kukamilika kwa miradi hiyo.



