CCM yaridhishwa ujenzi wa ofisi za watumishi Bukombe

GEITA: MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Geita, Nicolous Kasendamila ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa ofisi za watumishi wa umma katika Wilaya ya Bukombe.

Kasendamila ametoa kauli hiyo kwa niaba ya chama alipoongoza Kamati ya Siasa ya Mkoa kukagua ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri pamoja na ofisi mpya ya mkuu wa wilaya ya Bukombe.

Amesema maendeleo mazuri ya ofisi hizo mpya ni kiashiria cha uwajibikaji mzuri kwa watendaji wa serikali waliopewa dhamana ya kusimamia ujenzi wa miradi ya serikali.

Amesema ujenzi wa ofisi hizo ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita kuboresha mazingira ya huduma na utumishi katika ofisi za umma.

Amekiri kuwa wilaya hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikitumia ofisi zenye miundombinu isiyo rafiki na hivyo ukamilishaji wa ofisi mpya utakuwa kichocheo huduma bora kwa umma.

Mhandisi Msanifu Majengo wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Zahara Mawala amesema ujenzi wa ofisi ya mkuu wa wilaya Bukombe unatekelezwa kwa thamani ya Sh bilioni 3.27.

Amesema mpaka sasa mradi umefikia asilimia 83 ya utekelezaji ambapo jumla ya malipo ya sh bilioni 1.97 tayaru yameshafanyika.

Naye Mhandisi wa Wilaya ya Bukombe, Haruni Fashe alisema ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo unatekelezwa kwa gharama Sh bilioni 3.49.

Mhandisi Fashe amesema jumla ya fedha zilizopokelewa ni sh bilioni 1.88, fedha zilizotumika ni Sh bilioni 1.80 na tayari mradi umefikia asilimia 79.4 ya utekelezaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button